Vyama vya Siasa vyaaswa kushiriki uchaguzi wa Zanzibar - LEKULE

Breaking

27 Jan 2016

Vyama vya Siasa vyaaswa kushiriki uchaguzi wa Zanzibar

pic+jaji+mutungi
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe.Jaji Francis Mutungi. (Picha na Maktaba).

Na mwandishi wetu
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe.Jaji Francis Mutungi ameviasa Vyama vya Siasa kushiriki chaguzi zinazotangazwa na tume za uchaguzi nchini ikiwemo uchaguzi wa Machi 20, mwaka 2016 uliotangzwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
 Kwa mujibu wa barua iliyotolewa  kwa vyama hivyo leo na kusainiwa na  Jaji Mutungi  ilieleza kwamba,  kimsingi Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258 inasisitiza vyama vya siasa  kushiriki katika chaguzi zote zinazotangazwa na tume za uchaguzi ili kufikia malengo yake ya kushika dola.
“Katika nchi kidemokrasia na kwa chama cha siasa kinachoamini misingi ya kidemorasia ya vyama vingi vya siasa, hakuna njia mbadala kwa chama cha siasa kufikia malengo yake zaidi ya kushiriki uchaguzi.
“Ni wajibu wa kila chama cha siasa nchini  kama wakala wa kukuza demokrasia, utawala wa sheria na amani ya nchi, kuwa wa kwanza kutii matamko ya kisheria yanayotolewa na mamlaka  husika . Kama kuna chama cha siasa hakiridhiki au kimekwazwa kwa njia moja au nyingine na suala lolote kuhusu masuala ya uchaguzi, njia stahiki na inayonyesha ukomavu wa kisiasa si kuhamasisha kugomea uchaguzi, bali ni vema kikafuata utaratibu uliowekwa katika sheria za uchaguzi,” alisema Jaji Mutungi.
Aidha Msajili huyo amesema kwa mujibu wa Sheria za Nchi bado ni suala la hiari kwa chama kushiriki uchaguzi lakini utashi huo wa hiari unaenda sanjari na umuhimu wa kila chama kushiriki kila uchaguzi unaotangazwa na tume ya uchaguzi.
“Hivyo ni muhimu basi kila chama cha siasa kuelewa kuwa,uchaguzi ni kipimo cha uhai wa chama cha siasa. Chama cha siasa kisiposhiriki uchaguzi kinaua uhai wake katika mtazamo wa harakati za kisiasa,” alisisitiza.

Aliongeza kwamba hivi sasa, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na vyama vya siasa vimeimarika, hivyo sio vyema kwa chama cha siasa kujirudisha nyuma au kujiua kisiasa kwa kutoshiriki uchaguzi wakati kina uwezo wa kufanya hivyo.

No comments: