Umoja wa
Ulaya unasema mkataba wa eneo la Schengen, huenda ukasimamishwa kwa hadi
miaka miwili ikiwa utashindwa katika wiki chache zijazo kudhibiti
mmiminiko wa wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati na Afrika
Utekelezwaji
wa muda mfupi wa udhibiti wa mipaka ya eneo hilo utakamilika mwezi Mei.
Mawaziri wa uhamiaji wa serikali za Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini
Amesterdam wameamua kuwa mipaka huru ya Schengen huenda ikaendelea
kudhibitiwa kwa miaka miwili – hatua ya kurefushwa ambayo haikutarajiwa –
kwa sababu mzozo wa uhamiaji huenda usiweze kudhibitiwa ifikapo wakati
huo, kwa mujibu wa waziri wa uhamiaji wa Uholanzi, ambaye alikuwa
mwenyekiti wa mkutano huo.
Baadhi ya
mawaziri walieleza wazi kuwa hatua ya aina hiyo ya muda mfupi
kinadharia inaweza kuitenga Ugiriki, ambako zaidi ya watu 40,000
wamewasili kupitia baharini wakitoka Uturuki, licha ya makubaliano na
serikali ya Uturuki miezi miwili iliyopita yaliyoitaka izuie mmiminiko
wa wakimbizi wa Syria. Zaidi ya watu 60 wamekufa majini tangu Januari
mosi mwaka huu.
Maafisa
wa Ugiriki wamesema kuwa kufungwa njia hizo zinazotumiwa na wahamiaji,
hakuwezi kutatua tatizo hilo. Lakini shinikizo la wananchi kwa serikali
zao, ikiwa ni pamoja na nchi yenye nguvu kubwa kiuchumi katika Umoja wa
Ulaya, Ujerumani, kudhibiti na kupinga juhudi za kuwasambaza waomba
hifadhi kote katika umoja huo zinafanya sheria za usafiri huria
kutozingatiwa.
Kamishna
wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulos amezitaka nchi
wanachama kuzitekeleza hatua walizokubaliana kwa kudhibiti uhamiaji kote
barani huo – la sivyo mkataba wa eneo la Schengen uliodumu miaka 30
utaporomoka.
Lakini
waziri wa Uholanzi, Klaas Dijkhoff anasema muda umekwisha wa kuendelea
kuutekeleza mfumo huo ambao umewaruhusu mamia kwa maelfu ya watu
kutembea kwa miguu kutoka Ugiriki na Italia na kuingia Ujerumani na
Sweden katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kansela
wa Ujeruamani Angela Merkel, ambaye aliifungua mipaka ya nchi yake kwa
wakimbizi wan Syria, ana anakumbwa na shinikizo kubwa la kumtaka
asitishe mmiminiko huo, baada ya zaidi ya wahamiaji milioni moja kuingia
Ujerumani mwaka jana.
Umoja wa
Ulaya umechukua hatua kadhaa za kuipa Ugiriki inayokabiliwa na mgogoro
wa kifedha, msaada wa kifedha ili kukabiliana na mzozo wa wahamiaji,
lakini mataifa mengi wanachama wanaamini kuwa Athens haifanyi vya
kutosha. Umoja wa Ulaya sasa umependekeza kuzinduliwa kwa kikosi cha
pamoja cha walinzi wa pwani na mipaka ya Ulaya ili kuimarisha udhibiti
wa mipaka ya Umoja huo.DW(P.T)
No comments:
Post a Comment