UMOJA
wa Mataifa umeihadharisha Tanzania kuwa itakumbwa na mafuriko
yatakayosababishwa na mvua za El-Nino na kutaka kuanza kuchukua
tahadhari mapema.
Taarifa
ya Umoja huo ya uwezekano mkubwa wa mafuriko yatakayosababishwa na mvua
za El- Nino imetolewa wakati serikali inaendelea kubomoa nyumba
zilizojengwa maeneo hatarishi katika mabonde na maeneo yasiyoruhusiwa.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi anayehusika na
Misaada ya Kibinadamu na Uratibu wa Misaada ya Dharura, Stephen O’Brien,
Tanzania inaweza kukabiliwa na mafuriko ya El-Nino kati ya mwezi huu wa
Januari na Machi, mwaka huu.
Pamoja
na Tanzania, nchi nyingine ambazo zimetajwa kukumbwa na mafuriko hayo
makubwa ni pamoja na Madagascar, Malawi na Msumbiji.
Taarifa
ya O’Brien kuhusu madhara ya El-Nino na namna gani Jumuiya ya Kimataifa
inatakiwa kujiandaa au inajiandaa na kadhia hiyo iliwasilishwa mbele ya
wajumbe wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na nakala yake kutumwa
kwa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Pamoja
na kutoa tahadhari hiyo, O’Brien amezisihi nchi ambazo zinatarajiwa
kukumbwa na maafa ya El -Nino kujiandaa ipasavyo na kuyataja maandalizi
hayo kuwa ni pamoja na utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa wananchi
watarajiwa wa athari za mvua hizo.
Kwa
mujibu wa Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi, upande wa Afrika ya
Mashariki, nchi kadhaa hususan ukanda wa magharibi zimekumbwa na uhaba
mkubwa wa mvua na hivyo kuathiri kiwango cha upatikanaji wa chakula.
Nchi
hizo ni Ethiopia, Sudan, Djibouti na Eritrea ilihali baadhi ya nchi
zikipata kiwango cha mvua kilichovuka mipaka. “ Kuanzia mwezi Januari
hadi Machi, nchi za Tanzania, Msumbiji, Madagascar na Malawi zina
uwezekano mkubwa wa ku kumbwa na mafuriko ya El- Nino,” alisema O’Brien.
Alisema
nchi hizo zitahitaji pamoja na mambo mengine misaada ya kujiandaa na
kushughulikia kile kinachotabiriwa kwani kina uwezekano mkubwa wa
kutokea.
Ukiacha
nchi za Afrika ya Mashariki, nchi nyingine kwa upande wa Afrika ambazo
zimekumbwa na hali tete ya uhaba wa mvua na hivyo kutishia usalama na
upatikanaji wa chakula ni Angola, Botswana, Malawi, Namibia, Afrika
Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.
O’Brien
alisema nchi hizo zimekuwa na uhaba wa mvua kiasi kwamba zitakabiliwa
na uhaba mkubwa wa chakula na kusababisha watu zaidi ya milioni 28
katika mataifa hayo kukukosa chakula.
Akizungumzia
kuhusu misaada ambayo imekwishakutolewa na nchi wahisani ili kukabilia
na ukame na madhara yatokanayo na El-Nino , Katibu Mkuu Msaidizi
Mwandamizi huyo alisema kuwa hadi wakati anatoa taarifa yake kiasi cha
Dola za Marekani milioni 360 kilikuwa kimetolewa na wafadhili kwa lengo
la kukabiliana na madhara yatakayotokana na ElNino ikiwa ni pamoja na
usalama wa chakula.
Pamoja
na michango hiyo, O’Brien alisema haitoshi kutokana na ukweli kwamba
maafa yatakayotoka na madhila ya El-Nino yanahitaji misaada zaidi.
Mbali
ya nchi za kanda ya Afrika baadhi ya nchi nyingine ambazo zitakumbwa na
zilishawahi kupata balaa la El-Nino ni pamoja na nchi ambao zimo katika
Bara la Latini Amerika na nchi za eneo la Pasifiki ambazo nyingi ni
visiwa.
Shirika
la Kimataifa la Hali ya Hewa (WMO) linatarajiwa Mwezi Februari kutoa
taarifa zaidi kuhusu mwelekeo za mvua hizo za El-Nino.
Mvua
kama hizo zilishawahi kunyesha nchini Tanzania mwaka 1998 na
kusababisha maafa makubwa na watu kadhaa walipoteza maisha, huku maelfu
wengine wakijeruhiwa na kupoteza makazi.
Mwaka
jana mwezi Agosti Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa
tahadhari kuwa Tanzania ni kati ya nchi za Barani Afrika zitakazokumbwa
na mvua za El Nino kati ya mwezi Septemba na Desemba, mwaka jana.
No comments:
Post a Comment