TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MABADILIKO YA
MUUNDO WA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE
____________________
Kamati
ya Kanuni ya Bunge iliyoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mh. Job Ndugai hivi karibuni, leo imekutana Jijini Dar es
Salaam na Kuridhia mapendekezo ya mabadiliko katika muundo wa kamati za
Bunge yaliyowasilishwa na Mhe. Spika ili kuendana na mabadiliko ya
Muundo wa Wizara katika Serikali ya awamu ya Tano.
Mabadiliko
hayo ambayo yamefanywa chini ya kanuni ya 155 (3) ya kanuni za Kudumu
za Bunge yamezingatia madaraka aliyonayo Spika kufanya marekebisho
kwenye nyongeza za kanuni kwa kushauriana na kamati hiyo.
Akizungumza
na wajumbe wa kamati hiyo Mh. Ndugai ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati
hiyo amesema amelazimika kufanya mabadiliko katika muundo wa kamati ili
kuendana na mabadiliko ya Wizara na kwa kuzingatia kuwa muundo wa
kamati umetajwa kwenye nyongeza ya nane.
Katika muundo huo Kamati mbili mpya zimeundwa ambazo ni kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.
Akifafanua
kuhusu maamuzi ya Kikao hicho, katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah
amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio makubwa na kuridhia
mapendekezo ya Mhe. Spika kama yalivyowasilishwa.
Aidha
Dkt. Kashililah aliongeza na kusema kuwa Kamati nyingine zimefanyiwa
mabadiliko kwenye majina na nyingine mbili kuunganishwa na kufanya
kamati mpya za Bunge kuwa kama ifuatavyo:
Kamati zilizounganishwa ni:
- Kamati ya Huduma na maendeleo ya Jamii - imeunganishwa kutoka iliyokuwa Kamati ya Maendeleo ya Jamii na kamati ya Huduma za Jamii
- Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama – imeunganishwa kutoka iliyokuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama na kamati ya mambo ya Nje.
Kamati zilizofanyiwa Marekebisho madogo kwenye majina ni:
- Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira (awali ilikuwa Kamati ya Viwanda na Biashara)
- Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii (awali ilikuwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira)
- Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa (awali ilikuwa Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa)
Kamati zilizobakia kama ilivyokuwa awali ni pamoja na:
- Kamati ya Uongozi,
- Kamati ya Kanuni za Bunge,
- Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,
- Kamati ya Katiba na Sheria
- Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji,
- Kamati ya Miundombinu na
- Kamati ya Nishati na Madini.
Wabunge
wote wanatakiwa kuwasili Dodoma tarehe 20 Januari, 2016 tayari kwa
kuanza Vikao vya Kamati kabla ya Mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza
tarehe 26 Januari, 2016.
Imetolewa na,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano.
Ofisi ya Bunge,
S.L.P 9133,
DAR ES SALAAM
15 Januari, 2016.
No comments:
Post a Comment