MKURUGENZI
wa Kampuni ya Six Telecoms, Hafidh Shamte na wafanyakazi wengine
watano, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni nane.
Washitakiwa
walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka mawili na mawakili kutoka
Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Jackline Nyantori na Johanes Kalungura
wakisaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Theophil Mutakyawa, mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Mbali
na Shamte ambaye jina lake jingine ni Rashid, washitakiwa wengine ni
Ofisa Mkuu wa kitengo cha Fedha, Raphael Hongo, Mha sibu Said Ally,
Ofisa Masoko, Noel Chacha, Msimamizi wa mtandao, Tinisha Max na Mkuu wa
takwimu za biashara, Vishno Konreddy.
Akisoma
mashitaka, Jackline alidai, katika tarehe tofauti kati ya Mei 2010 na
Januari mwaka huu, Dar es salaam, kwa lengo la kujipatia fedha,
washitakiwa walitoza huduma za simu za kimataifa chini ya dola za
kimarekani senti 25 kwa dakika.
Wakili Jackline, alidai jambo hilo lilisababisha washindwe kuilipa TCRA, mapato ya dola za Marekani milioni 3,836,861 zilizopatikana kutokana na huduma za simu za kimataifa zilizokuwa zinaingia.
Katika
mashitaka mengine ilidaiwa, katika tarehe hizo, kutokana na kutoza
chini ya dola za kimarekeni senti 25 kwa dakika na kushindwa kuilipa
TCRA mapato yanayotokana na huduma hiyo, waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya dola za kimarekani 3,836,861, sawa na Sh bilioni nane za kitanzania.
Wakili Jackline alidai, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Awali,
kabla washitakiwa hawajasomewa mashitaka, Hakimu Mwijage aliwaambia
washitakiwa hawaruhusiwi kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina
mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu, au endapo
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atatoa kibali kwa mahakama hiyo kusikiliza
kesi hiyo.
Aidha
alisema mahakama haiwezi kutoa dhamana, hivyo wapeleke maombi ya
dhamana Mahakama Kuu. Washitakiwa walirudishwa rumande na kesi hiyo
iliahirishwa hadi Janurai 28 mwaka huu itakapotajwa tena.
Wakati
huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
Johanes Kalungura ametoa siku saba kwa Bodi ya waku rugenzi wa kampuni
ya Six Telecoms Tanzania Limited, kuilipa mamlaka hiyo deni la Sh
bilioni nane.
Kalungura
alisema hayo jana, Dar es Salaam, akiwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu baada ya kuwafikisha mahakamani wafanyakazi watano wa kampuni
hiyo kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni nane.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kalungura alisema “Naomba
wakurugenzi wote au bodi ya wakurugenzi walipe fedha za wananchi,
shilingi bilioni nane ndani ya siku saba kuanzia leo (jana), wasipofanya
hivyo sheria itachukua mkondo wake dhidi yao” .
Aidha
aliwakumbusha wamiliki wa makampuni yote yanayotoa huduma za
mawasiliano, ambao wanajua hawajalipa tozo za nchi, walipe haraka kwa
sababu wasipolipa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment