Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia
Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora alifanya ziara ya kutembelea Shirika
la Posta Tanzania ili kufahamu utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu
ya Shirika.
Katika
ziara hiyo Prof. Kamuzora aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt.
Maria Sasabo na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Shirika hilo.
Katika ziara hiyo Prof. Kamuzora alimuagiza Kaimu Posta Masta Kuu wa Shirika la Posta Tanzania Ndugu Fortunatus Kapinga kuhakikisha
kuwa ukusanyaji wa mapato yote ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) nchi
nzima yanafanyika kwa kutumia njia ya elektroniki ambapo alisema kuwa, “Shirika
liboreshe mifumo yake ya kielektroniki ili kupunguza mianya ya wizi na
upotevu wa fedha za Shirika na kufanikisha ongezeko la ukusanyaji wa
mapato ya Serikali”.
Prof.
Kamuzora aliongeza kuwa Shirika la Posta Tanzania liendane na
mabadiliko ili liende kuwahudumia wananchi wa sasa na wa vizazi vijavyo.
Shirika ni la kipekee na lina nafasi nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi
kama ambavyo Shirika kama hili linafanya kazi nzuri kwenye nchi ya
China na Brazil.
Aidha,
Prof. Kamuzora aliwaagiza Viongozi wa wasimamizi wa Shirika la Posta
Tanzania kutumia Sheria, Kanuni na taratibu za kuwasimamia wafanyakazi
na kuwachukulia hatua kali na za kinidhamu watumishi wazembe;
wasiotimiza majukumu yao; wasio waaminifu na wabadhirifu.
Aliongeza
kuwa watendaji wafanye kazi na kusimamia Shirika kwa kuwekeana malengo
kama inavyojulikana kisheria kwa kutumia Mfumo wa wa Wazi wa Upimaji
Utendaji Kazi (OPRAS).
Alisisitiza kuwa, “Sheria
zilizopo zinatosha kumsimamisha mtumishi kazi kwa makosa na hatimaye
kumfukuza kazi kwa kuwa watumishi wazembe na wasio waadilifu wanawafanya
wananchi wawe na mtazamo hasi na Serikali yao”.
Prof.
Kamuzora alisema kuwa wateja wanahitaji huduma nzuri; ya uhakika na
kufikishiwa vifurushi, barua, vipeto na bidhaa nyingine kwa wakati.
Aliwaagiza
viongozi wa Shirika kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za
uendeshaji ili kuendesha Shirika kwa tija na faida. Prof. Kamuzora
alisema, “Uchumi wa nchi hauwezi kukua wala kwenda popote bila kufanya kazi kwa tija."
Alivitaka
vyama vya wafanyakazi visiwatetee watumishi wazembe na vishirikiane na
Serikali kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika na watumie
mtandao mpana wa Shirika uliopo nchi nzima na kuangalia fursa zilizopo
ili kufikisha huduma kwa wateja.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Mawasiliano ambaye
aliambatana na Katibu Mkuu wake Dkt. Maria Sasabo aliagiza kuwa, “Shirika
lijipange haraka na kuongeza kasi ya utendaji kazi ya kuwahudumia
wateja wake na wananchi ili kuweza kuendana na Serikali ya Awamu ya Tano
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli”.
Dkt.
Maria Sasabo aliongeza kuwa Shirika la Posta lipo nchi nyingi duniani
na bado linahitajika hivyo ni muhimu kujipanga kuendana na mahitaji ya
sasa ya wateja na Shirika libadilishe utaratibu wa utendaji kazi na
kuondoa urasimu ili kuweza kuwahudumia wateja.
Dkt.
Maria Sasabo aliwaagiza viongozi wa Shirika wafanye tathmini na
kuangalia namna bora ya kujiendesha ikiwemo kupitia upya muundo na
majukumu ya Shirika.
Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Kamuzora
aliuagiza uongozi wa Shirika la Posta Tanzania kuongeza matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kuwa na huduma za ziada za
kisasa zinazoendana na mahitaji ya wateja kwa kutumia biashara mtandao
kusafirisha na kufanikisha usambazaji wa huduma na bidhaa za wateja kama
vile uagizaji wa magari; vitabu na bidhaa nyingine kwa kushirikiana na
kampuni kubwa duniani kama vile Alibaba, Amazon na eBay.
Imetolewa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
No comments:
Post a Comment