Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
ametoa siku 30 kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
(Nacte), Dk Primus Nkwera kufanya ukaguzi wa vyuo vyote na kumkabidhi
ripoti ili kujiridhisha na ubora wa elimu inayotolewa.
Pia,
amewataka watendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuandaa mitalaa
yenye matokeo ya kujenga wanafunzi watakaozalisha kwenye jamii.
Waziri
huyo ambaye amewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta), alitoa maagizo hayo jana wakati wa ziara yake katika ofisi
hizo ikiwa ni siku tano baada ya kuapishwa kuiongoza wizara hiyo.
Alisema anawafahamu vyema watendaji wote wa taasisi hizo na hatavumilia kuona ubora wa elimu ukiendelea kuporomoka nchini.
Aliitaka
TET kuhakikisha mtalaa wa KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu) kwa darasa
la kwanza na la pili unapelekwa shuleni kabla ya Januari 13.
“Lakini
pili, ningependa muanze kutumia walimu wastaafu kwenye uandaaji mitalaa
hiyo na ukaguzi uimarike kwa wanafunzi, mnaweza kuwa na mitalaa mizuri
lakini ufuatiliaji ukikosekana haitasaidia,” alisema.
Kuhusu ubora wa elimu alisema: “Ningependa
uonekane kwa matokeo baada ya kumaliza shule, sihitaji kusikia amefaulu
kwa alama ngapi ila amejengewa uwezo gani kichwani,” alisema.
Alisema kasi ya uwajibikaji TET imekuwa ndogo kwani kitabu cha kurasa 16 kinatengenezwa kwa mwaka mmoja.
“Ninaweza kuja hapa mnipatie nafasi halafu tujipime na nyie tuone, naomba mbadilike nimeona mko nyuma sana ya kasi yangu,” alisema.
Mbali
na maagizo hayo, Profesa Ndalichako aliiagiza Nacte kufanya usajili wa
vyuo kwa kuzingatia mahitaji ya soko badala ya kusajili holela bila
ufuatiliaji kwa kuwa baadhi vinajiendesha kwa ujanja ujanja.
Alisema
suala la ubora wa elimu linamkosesha usingizi. Alilitaka baraza hilo
kungeongeza kasi ya ushawishi katika uwekezaji wa shule za ufundi badala
ya kujikita kwenye upandishaji wa hadhi ya vyuo na kuondoa dhana ya
biashara katika sekta ya elimu.
“Lakini
pia ningependa wafanyakazi wote mbadilike, tuache kufanya kazi kwa
mazoea. Katika upandishaji hadhi ya vyuo, lazima tujiridhishe na
mahitaji ya Taifa, pia kwa suala la udahili wa wanafunzi, ningependa
vyuo ambavyo havijatambuliwa kwenye mfumo wa Necta viingizwe ili kuondoa
udanganyifu wa vyeti wa usajili,” alisema.
No comments:
Post a Comment