Dk Harrisson Mwakyembe atembelea Tume ya Haki za Binadamu - LEKULE

Breaking

1 Jan 2016

Dk Harrisson Mwakyembe atembelea Tume ya Haki za Binadamu



Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dk Harrisson Mwakyembe ameitembelea  Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kusema kuwa ni  chombo muhimu ambacho uwepo wake unaipa heshima kubwa Tanzania kimataifa.

Akizungumza katika ziara aliyoifanya katika Ofisi za Tume jijini Dar es Salaam tarehe 31 Desemba 2015, Dk Mwakyembe alisema Tume ni chombo muhimu kwa taifa kilichoanzishwa kikatiba kwa lengo la kulinda na kutetea haki za binadamu nchini.

"Wananchi tunaowaongoza wanakihitaji hiki chombo kwa kuwa kimeundwa kusimamia haki zao" alisema Dk Mwakyembe

"Chombo hiki kipo kwa ajili ya kusimamia masuala ya haki za binadamu, serikali wakati mwingine katika kutekeleza majukumu yake yanaweza kutokea mapungufu ya kiutendaji, hivyo Tume ipo kwa ajili ya kurekebisha mapungufu hayo ili nchi iende vizuri" aliongeza

Dk Mwakyembe alisisitiza kuwa Tume inachokifanya ni katika mipango ya Serikali, na kwa hakika inaisaidia serikali iende katika mstari unaotakiwa.

Aidha, Dk Mwakyembe alitumia fursa hiyo kuwapongeza wafanyakazi wa Tume kwa uzalendo na uadilifu wao katika kazi waliouonesha na amewaahidi kushirikiana nao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.


Akizungumza mapema, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Bahame Nyanduga alimueleza Waziri, Dk Mwakyembe kuwa pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na Tume katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ya kila siku bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya rasilimali fedha na uchakavu wa vitendea kazi.

No comments: