Hivi kitendo cha Ukawa kutomtambua Rais si jipu? - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Wednesday, 13 January 2016

Hivi kitendo cha Ukawa kutomtambua Rais si jipu?


Uchaguzi Mkuu uliopita ambao Dk John Pombe Magufuli ameshinda na kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, ulikuwa na ushindani mkubwa ambao kwa mara ya kwanza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeonja ‘uhalisia’ wa ukali wa siasa za vyama vingi.
Kwa safari hii, CCM ilipambana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kiliungwa mkono na vyama vingine vitatu ambavyo kwa pamoja vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Pamoja na mgombea Urais wa CCM kushinda na kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa mshindi na hatimaye kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bado mpaka leo hii aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho, hawajanukuliwa kukubali matokeo ya uchaguzi huo, na hapo ndipo ninapoleta tafakuri ili tutafakari pamoja kwamba hilo nalo siyo ‘jipu’ miongoni mwa majipu yanayohitaji kutumbuliwa?
Ni vizuri Watanzania tukakumbushana kwamba mfumo huu wa demokrasia ya ‘wengi wape’, vyama vyote vya siasa nchini vilisaini makubaliano ya uendeshwaji wa uchaguzi kwa misingi iliyokubaliwa kati ya vyama hivyo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Si vyema kusahau msingi wa ukimya wa aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema pamoja na Mwenyekiti wake juu ya kutotamka hadharani kukubali matokeo ya uchaguzi au kutamka kumkubali mshindi wa kiti cha urais wa Tanzania katika uchaguzi huo, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli.
Chimbuko lake ni kwamba alinukuliwa Mwenyekiti wa Chadema wiki chache kabla ya uchaguzi akilalamikia kitendo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya nne, Mheshimiwa Dokta Jakaya Mrisho Kikwete, kumbadilisha Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, jambo ambalo lilimghadhibisha sana Mwenyekiti huyo hadi kufikia kumtamkia mteuliwa huyo wa Rais kwamba ameteuliwa ili kufanikisha wizi wa kura.
Kauli hiyo ya Mwenyekiti wa Chadema ilimaanisha tafsiri mbili: Tafsiri ya kwanza ni kwamba Mwenyekiti huyo alishapoteza imani na NEC mapema kabla ya uchaguzi kufanyika. Na tafsiri ya pili ni usiri wa Mwenyekiti huyo usio na tafsiri rasmi juu ya kuwa na imani na Mkurugenzi aliyeondolewa, na huku akipoteza imani na Mkurugenzi mpya.
Tusisahau pia kwamba aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema aliwahi kutamka hadharani katika mahojiano maalum kwamba atayakubali matokeo ya urais endapo uchaguzi utakuwa huru na haki; kauli ambayo haina tafsiri nyingine zaidi ya kwamba uchaguzi kuwa huru na haki ni yeye kushinda.
Kwa muktadha huo, ni juu yetu wanatafakuri kuijadili kadhia hii ya Mwenyekiti wa Chadema kutomtambua Rais halali aliyeko madarakani na ambaye amepatikana kwa misingi ya kikatiba na kutambua ni nini hatma ya wafuasi wao kama nao wanamkubali au laa.
Ni muhimu pia kukumbushana kwamba Chadema kutokana na idadi ya Wabunge wake kinakuwa ndiyo chama kikuu cha upinzani kwa sasa kitakachounda kambi rasmi ya upinzani Bungeni. Je, hilo litatimia vipi kama kiongozi mkuu wa chama hamtambui Rais wa nchi?
Ukimya tulio nao Watanzania juu ya kadhia hii nyeti ya kuwapo viongozi ambao wanategemewa lakini hawamtambui Rais aliyeko madarakani, sijui demokrasia tunaipa tafsiri gani? Hivi tafsiri ya demokrasia ni uhuru wa kumkataa Rais aliyepatikana kikatiba? Na Je, kitendo cha hawa walioshindwa kwa idadi kukataa maoni ya kupitia sanduku la kura yaliyompa ushindi aliyeshinda, hiyo nayo ni demokrasia?
Lakini kama tutaendelea kukaa kimya kisha ukaja kuzaliwa mgongano wa kimamlaka kwamba Mheshimiwa Rais anaamrisha jambo na Mwenyekiti ambaye bado hajamkubali Rais anataka kufanya kinyume chake; Je, huyu raia mnyonge atashika upande gani?Hivi kwani tumesahau matokeo ya huko nyuma yaliyosababishwa na mgongano wa kimamlaka pale Jeshi la Polisi lilitoa amri ya kukataza maandamano lakini kiongozi wa chama cha siasa akapingana na amri hiyo na akawaamrisha wafuasi kuandamana na hatimaye raia kadhaa waliathirika na hata wengine kupoteza maisha kabisa?
Ukweli lazima usemwe hata kama ni mchungu! Siyo sahihi hata kidogo kuruhusu kiongozi wa kundi fulani ‘aingilie’ mamlaka kwa kumkataa Rais aliyepatikana kupitia sanduku la kura kwani huko ni kutoheshimu zile kura za wengi waliompa ushindi Rais huyo, na hapo sasa ndipo unapofunguliwa mlango wa kuikataa demokrasia ya ‘wengi wape’?
Sasa mjadala upo wazi! Mtanzania ambaye mpaka wakati huu anakataa kumtambua Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli kama Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hoja yake kuu ni kwamba mikutano yake ilijaza sana washabiki na kutokana na hilo ni yeye ndiye aliyeshinda katika uchaguzi huo; hivi hata kama pengine kadhia hiyo siyo ‘jipu’ basi haiwezi kuwa hata ‘kipele’? Vipi tunakaa kimya katika kadhia ya hatari kama hii?
Nihitimishe tafakuri kwa kumuomba aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema atamke hadharani kumkubali Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli, kwa sababu zifuatazo:
(1) Ni uamuzi wa kikatiba kwamba anayetangazwa na NEC kuwa mshindi, ushindi wake hauhojiwi popote hata mahakamani. Kuendelea kubakia kimya siyo ustaarabu wa Kitanzania.
(2) Kwa kuwa yeye ni Waziri Mkuu mstaafu na anazo stahiki zake kutoka serikalini, si vyema kuzipokea stahiki hizo na ilihali Serikali inayokupa humtambui mkubwa wake.(3) Ni vizuri pia kutoamini idadi kubwa ya waliohudhuria mikutano yako ya kampeni walipiga kura kwani ni siri ya mtu na wengi wao hawakujiandikisha, walikata tamaa kwamba wapinzani hawana mgombea mwenye mvuto.
Ikumbukwe kujiandikisha Daftari la Kudumu la Wapigakura kulipita ndiyo akapatikana mgombea mwenye ‘mvuto’ wa upinzani, hali iliyopelekea kupata hamasa. ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wakati muda wa kujiandikisha ushapita na hivyo kukosa sifa ya kupiga kura.
(4) Chama ambacho umekitumia si chama salama kwani kilishabebeshwa tuhuma nyingi tena na aliyekuwa mtendaji wake mkuu (katibu mkuu) na hivyo kisingeweza kupata nguvu ya kushinda.
(5) CCM ‘iliotea’ kumsimamisha mgombea ambaye sifa zake na uchapakazi wake unakubalika na Watanzania wote, wale wa CCM na wasiokuwa CCM. Na ndio maana wakati wa kampeni hofu kubwa iliyojengeka kwa wapiga kura ilikuwa ni iwapo ‘mfumo wa CCM’ utamuacha mgombea huyo aongoze bila ya kumfanyia ‘mizengwe mizengwe’ ya ki-CCM, jambo ambalo kwa sasa tayari limeshabainika kwamba ilikuwa ni ‘shaka’ tu ambayo haina msingi wowote wa ushahidi.
Haya tukubalianeni basi kwamba wale wasiomtambua Mheshimiwa Rais, John Pombe Magufuli, mpaka wakati huu nao ni ‘jipu’ linalohitaji kutumbuliwa.
Haya na tutafakari.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa ARRISAALAH ISLAMIC FOUNDATION.Unaweza kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749.
Post a Comment