Timuatimua ya mawaziri yakosolewa - LEKULE

Breaking

13 Jan 2016

Timuatimua ya mawaziri yakosolewa


Dar es Salaam. Wasomi nchini wamekosoa hatua ya baadhi ya mawaziri kuwasimamisha kazi watendaji wa Serikali kutokana na sababu mbalimbali wakisema si dawa ya kurejesha utumishi uliotukuka bali kinachotakiwa ni kuweka mfumo imara wa utawala.
Katika mahojiano na Mwananchi, wasomi hao wamesema baadhi ya mawaziri wanachukua hatua hizo ili waonekane wachapa kazi lakini ukweli wanachukua uamuzi bila kuwasikiliza wahusika, kufanya utafiti wa kina wala kujua changamoto zinazowakabili.
Tangu walipoapishwa Desemba 23, 2015, baadhi ya mawaziri wamekuwa wakifanya ziara za kushtukiza, kutoa matamko na maagizo kwa watendaji wa Serikali, ambapo mpaka sasa zaidi ya watendaji 20 wa Serikali, mashirika na taasisi zake wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Baadhi ya waliosimamishwa ni Ofisa Biashara Manispaa ya Ilala, Dennis Mrema kutokana na agizo lililotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi, George Simbachawene Januari 7, baada ya kutuhumiwa kusababisha upotevu wa mapato kwa Serikali.
Januari 5, Waziri wa Masiliasi na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango wa Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohammed Kilongo na maofisa misitu wa mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.
Pia, Rais John Magufuli katika siku 70 za utawala wake ameshawatimua kazi wafanyakazi 70 wakiwamo watumishi na wajumbe wa bodi wa mashirika au taasisi husika wakidaiwa ama kushindwa kuwajibika au kutosimamia vizuri maeneo yao.
Walioangukiwa na rungu la Rais Magufuli ni watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Wizara ya Uchukuzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohamed Bakari alisema kama hakutafanyika mabadiliko katika mifumo ya uendeshaji katika taasisi na ofisi mbalimbali za umma hakutakuwa na mabadiliko ya maana yatakayofanywa na mawaziri hao.
Bakari alitolea mfano utendaji wa Mamlaka ya Bandari na TRA, akisema mfumo wa utendaji ni ule ule, hivyo hata akiwekwa ‘mtendaji aliyetukuka’ mambo yanaweza kuwa yaleyale kwa sababu utaratibu wa uendeshaji wa bandari umeachwa kama ulivyokuwa awali.
Kuhusu sakata la makontena kupitishwa bandarini bila kulipiwa kodi na tozo mbalimbali, Bakari alisema wengi wanaopitisha mizigo ni wanasiasa, jambo ambalo huwafanya wafanyakazi wa bandari kuwa wepesi wa kukubali mizigo hiyo kupita bila kulipiwa chochote kwa kuhofia usalama wa kibarua chao.
“Kuwawajibisha ni sawa, sasa tujiulize kuna mabadiliko ya mfumo ili kuwatengenezea mazingira ya kufanya kazi bila kuingiliwa na mtu?” alihoji Bakari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP), Lilian Liundi alisema kabla ya kwenda mahali popote penye tatizo na kutoa tamko au kusimamisha watu kazi, mawaziri wanatakiwa kufanya utafiti wa kina ili kujiridhisha.
Alisema wanachofanya hakina tatizo iwapo tu kitafanywa kwa haki kulingana na ushahidi na vithibitisho walivyonavyo ili kuchukua uamuzi ambao hautalalamikiwa na wahusika.
Alisema licha ya kuwa watumishi wengi wa umma walifanya kazi kwa mazoea, kuna njia nyingi za kurejesha utumishi bora, si lazima watu kusimamishwa kazi au kufukuzwa.
“Kama utafiti utafanyika na kubainika ukweli waadhibiwe tu, hapo hakuna majadala kwa sababu uzalendo, uwajibikaji, kujituma kulipotea kabisa. Watumishi wa umma walikuwa wanafanya kazi kwa mazoea, hiyo inaweza kuwa ndiyo sababu kubwa ya haya yanayotokea sasa, ” alisema Liundi.
Mkurugenzi wa utetezi na maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema kinachoendelea sasa ni aina mbili za uwajibishwaji. Kwanza ni ule aliosema hana shaka nao ambao ni wahusika kuwajibishwa kwa makosa waliyoyafanya kwa bahati mbaya au makusudi.
Pili, alisema ni uwajibishwaji unaohusisha visasi vya kisiasa au binafsi. “Yaani mwenye nafasi au cheo hutumia nafasi hiyo kumwadhibu mwenzake hata kama hana hatia kwa sababu tu ana uwezo wa kufanya hivyo, huo ndiyo wenye shida.” Alisema pamoja na viongozi kuwa na haki kisheria ya kuwaadhibu wanaokiuka maadili ya utumishi, lakini kuna haki ya msingi kwa kila anayetuhumiwa kujieleza au kujitetea.
Alisema kisheria kumwadhibu mtu bila kumsikiliza hata kama kuna ushahidi wa kutosha ni kosa, lazima apewe nafasi ya kujitetea kwa maelezo kuwa pengine alikuwa na sababu za kufanya hicho alichokifanya.


Alisema anaunga mkono juhudi zinazofanywa sasa kwa watumishi wa Serikali kutokana na mazoea na uzembe uliokithiri huku akisisitiza kuwa kutoa nafasi kuwasikiliza wahusika, kufanya uchunguzi wa jambo kabla ya kutoa uamuzi, ni masuala ya msingi yanayopaswa kufanywa na mawaziri. 

No comments: