Polisi inatoa ulinzi katika eneo kulikotokea mlipuko karibu na eneo takatifu la St Sophia na Msikiti wa Blu, Januari 12, 2016.
Na RFI
Mlipuko
mkubwa umetokea Jumanne hii Januari 12, 2016 katika kituo cha utalii cha
Sultanahmet katika mji wa Istanbul, karibu na Msikiti wa Blu na
makavazi ya St Sophia.
Watu
wasiopungua 10, wengi wao wakiwa Wajerumani wameuawa, na wengine 15
wamejeruhiwa. Waziri mkuu amesema kuwa mshambuliaji, ni raia wa Syria,
ambaye alizaliwa mwaka 1988, na ni mwanamgambo wa kundi la Islamic
State.
Shambulio
lililotokea Jumanne hii asubuhi limeligusa eneo lenye ishara kubwa
katikati mwa mji wa Istanbul, eneo ambalo ni la kitalii la Sultanahmet.
Kwa mujibu wa mwandishi wetu katika mji wa Istanbul, Alexander Billet,
mlipuko huo ulikua mkubwa kwani ulisikika hata katika miji mbalimbali
jirani barani Asia.
Waathirika wengi ni Wajerumani
Vyombo
vya habari vya Uturuki awali vilibaini kuwa watu kadhaa walijeruhiwa,
wala hakuna aliyepoteza maisha, lakini mlipuko huo umesababisha vifo vya
watu wasiopungua 10. Wengi wa watu waliopoteza maisha ni wageni. Mapema
mchana, Waziri mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, amewasiliana na
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ili kumuarifu kuwa wengi mwa
waliopoteza maisha ni raia wa Ujerumani. Wizara ya mambo ya nje ya
Ujerumani imewashauri raia wake kuepuka maeneo ya kitalii ya Istanbul.
Ubalozi wa Norway umesema kuwa mmoja wa raia wake ni pia miongoni mwa
watu waliopoteza maisha.
Waziri
mkuu Ahmet Davutoglu ameendesha mkutano kuhusu hali hiyo Jumanne hii
asubuhi na waziri wa mambo ya ndani pamoja na mkuu wa Idara ya Ujasusi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri mkuu wa Uturuki Numan Kurtulmus, mamlaka ya
nchi hiyo imemtambuliwa muhusika wa shambulio hilo, mshambuliaji wa
kujitoa mhanga anayeelezwa kuwa ni raia wa Syria, ambaye alizaliwa mwaka
1988. Katika hotuba fupi kwenye runinga ya taifa, Ahmet Davutoglu
amesema kuwa ni mwanamgambo wa kundi la Islamic State. Mapema mchana,
wakati wa hotuba yake kwa taifa, rais wa Uturuki mwenyewe amelaani
"shambulio hilo la kujitoa mhanga".
No comments:
Post a Comment