NMB na John Deere wasaini makubaliano Kusaidia Wakulima Nchini - LEKULE

Breaking

22 Jan 2016

NMB na John Deere wasaini makubaliano Kusaidia Wakulima Nchini

NMB (1)
Nmb
Dar es Salaam – Januari 21, 2016: Kampuni maarufu kwa uuzaji wa matrekta duniani ya John Deere imeingia makubaliano na benki ya NMB ili kutoa mikopo nafuu kwa wakulima wanaochipukia nchini yenye nia ya kuwarahisishia kupata vifaa vya kilimo.
Makubaliano hayo yatarahisisha upatikanaji wa vifaa kazi kama matrekta kutoka kampuni ya John Deere kupitia wakala wao wa hapa nchini – LonAgro ambao husambaza matrekta kwaajili ya shughuli za kilimo.
Kupitia makubaliano hayo yaliyoingiwa jana jijini Dar es Salaam, nje ya kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya kilimo, pia kampuni ya John Deere itatoa mafunzo ya jinsi ya kutumia vifaa hivyo hayo pamoja na mafunzo ya biashara ya kilimo kwa wanunuzi wa vifaa hivyo.
NMB (3)
Mkurugenzi wa John Deere kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara – Antois van der Westhuizen amesema kuwa mikopo hiyo ya matrekta itakayotolewa na NMB kwa kushirikiana na kampuni yake  ina lengo la kuinua wakulima wadogo kubadirisha kilimo kutoka kilimo cha mazoea kuwa kilimo endelevu chenye kutumia vifaa vya kisasa kama matrekta ya kulimia, kuvuna na pia kusafirisha mazao.
“kwa kutambua umuhimu wa wakulima wadogo katika nchi za Afrika, John Deere kwa kushirikiana na NMB tunategemea kuweka mifumo itakayowawezesha wakulima wadogo ili kuleta ufanisi katika shughuli nzima za kilimo. Ufanisi katika manunuzi ya pembejeo, uzalishaji na pia matumizi ya teknolojia za kisasa (mbegu, mbolea na hata vitendea kazi – Mashine) na pia ufanisi katika kutafuta masoko ya mazao shamba yao.” Alisema van der Westhuizen na kuongeza kuwa John Deere inaelewa kuwa wakulima wadogo wanaweza wasimudu uwekezaji wa tekinolojia na ndio maana wapo NMB kusaidia kuwapa mikopo itakayowawezesha kununua vifaa hivyo.
NMB (2)
Uwezeshaji kutoka kwenye taasisi ya fedha utasaidia wakulima wengi kumudu upatikanaji wa vifaa muhimu vya kilimo kulingana na tekinolojia za kisasa za kilimo na hivyo kusaidia kuboresha shughuli za wakulima mashambani, kuongeza mavuno na pia kuongeza kipato cha kaya moja moja.
“malengo makubwa ya John Deere ni kusaidia wakulima wadogo na wanaochipukia kufanya kilimo kama biashara na kukuza shughuli hizo mpaka kufikia kuwa wajasiliamali wakubwa watakaosaidia wakulima wadogo kupitia vifaa vyao vya kilimo kama matrekta ya kulimia na kuvuna kupitia mtindo wa mkataba.” Aliongeza  van der Westhuizen
Akiongea baada ya kuweka saini makubaliano jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha wateja wakubwa wa NMB – Filbert Mponzi alisema kuwa benki inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa nchi na hivyo kuchukua hatua madhubuti ya kuingia makubaliano na makampuni na pia kubuni bidhaa zinazolenga kuboresha sekta ya kilimo.
“upatikanaji wa mikopo, siku za nyuma ulikuwa ni kikwazo kikubwa katika maendeleo ya kiilimo, makubaliano haya yanakuja kuleta suruhisho muhimu kabisa kwa wakulima kuanza kumudu gharama za ununuzi wa vifaa muhimu vinavyoendana na tekinolojia ya leo katika kilimo.” Alisema Bwana Mponzi.
NMB tumewafikia zaidi ya wakulima wadogo 600,000 kwa kusaidia mitaji kwaajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, pia tunasaidia wakulima wakubwa ili waweze kukua zaidi. Katika mipango ya benki ya uwajibikaji kwa jamii, tunatoa elimu kwa wajasiliamali kupitia mafunzo mbalimbali ya kibiashara na hivyo kuwawezesha kwa maarifa na uelewa jinsi ya kutunza fedha na pia kukuza mitaji.
Kampuni ya John Deere inaamini kuwa wakulima wanaochipukia kwa kutumia mashine ambazo zinawawezesha kufanya kilimo cha kisasa kwa kupitia mafunzo maalumu, wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa hazina ya chakula duniani. Wanaamini kuwa wakulima wadogo na wanaochipukia kwa kutumia vifaa vya uhakika na mafunzo watachangia sana kuongezeka kwa mavuno na uzalishaji kukua mara dufu katika mtiririko mzima wa mzunguko wa kilimo nchini.
LonAgro, kama mawakala waliosajiliwa na John Deere nchini, wanaamini kuwa suruhisho la zana za kilimo na mashine ndilo suruhisho pekee katika kukabiliana na upungufu wa chakula duniani.

Mkurugenzi wa LonAgro Tanzania Lukas Botha alisema kuwa “Kupitia makubaliano kati ya NMB na John Deere, wakulima wana uhakika wa kupata nyenzo muhimu na kufanya ukulima kwa tekinolojia kisasa kuwezekana na pia wana uhakika wa kupata ushirikiano mkubwa kutoka LonAgro na kufanya mashirikiano endelevu.”

No comments: