ABIRIA 269 waliokuwa wakisafiri kutoka Mwanza kuelekea wilayani Bukoba, wamenusurika kufa baada ya meli ya Mv Serengeti waliokuwa wakisafiria kupata hitilafu ya injini katika ziwa Victoria.
Meli
ya Mv Serengeti ambayo muda sio mrefu ilitoka katika matengenezo,
katikati ya mwaka jana ilipata hitilafu kama hiyo ikiwa ziwa Victoria na
abiria kitendo ambacho kinaelezwa kuwapa wasiwasi watumiaji wa chombo
hicho.
Meli
hiyo iliyokuwa na abiria 269, tani 64 za mizigo pamoja na gari ndogo,
ilipata hitilafu kwenye mfumo wa shafti na majembe ya upande wa kulia
(Starboard side) ambayo yalisababisha meli hiyo kuchelewa kutia nanga
katika Bandari ya Bukoba.
Akizungumza
leo na waandishi wa habari mjini hapa, Kaimu Meneja wa Kampuni ya
Usafirishaji Majini, Kapteni Winton Mwassa, amesema meli hiyo iliondoka
juzi kutoka Mwanza saa 12 : 40 jioni na kutia nanga jana saa 6: 05
mchana na kwamba ilipata hitalafu majira ya saa 6:20 usiku.
Amesema
kuwa mpaka sasa chanzo cha meli hiyo kuchelewa kutia nanga bado
hakijafahamika na kwamba walipata taarifa kutoka kwa Nahodha wa Meli
hiyo, Bembele Ng’wita kwamba mfumo wa shafti na majembe ya kulia ya
upande wa kulia yamepata hitilafu.
“Kwa
mujibu wa taarifa ni kwamba saa 6:20 usiku mfumo huo ulipata hitilafu
iliyopelekea injini kuwa nzito na kusababisha meli kutetemeka na joto la
injini kupanda na kupelekea injini hiyo kuzimwa kwa usalama zaidi,” amesema Mwassa.
Hata
hivyo amesema baada ya hali hiyo meli iliiendelea na safari yake kwa
kutumia injini moja na kwamba imewasili salama katika Bandari ya Bukoba
saa 6: 05, abiria wote na mali zao wapo salama.
Amesema
baada ya kupata taarifa hizo, kampuni imemtuma mpiga mbizi (Diver) kwa
usafiri wa ndege ili akakague mfumo huo na kuweza kubaini tatizo na
chanzo cha kusababisha hitilafu hiyo na kwamba kwa mujibu wa Nahodha
huenda meli ilinasa katika nyavu za wavuvi.
Mwassa
aliwataka watanzania kutokuwa na wasiwasi na usafiri huo na kuwataka
kuondoa zana potofu kwamba watumishi wa meli hiyo wanauhujumu usafiri wa
meli zinazomilikiwa na Serikali kitendo ambacho alikikana.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, alipotafutwa kuzungumzia
tukio hilo hakupatikana ofisini kwake na kwamba yupo nje ya ofisi.
No comments:
Post a Comment