"Mimi ndiye Rais Halali wa Zanzibar na Nisiposema Mimi Nitawatuma Wasaidizi wangu Kuwaeleza" - Dk Shein - LEKULE

Breaking

7 Jan 2016

"Mimi ndiye Rais Halali wa Zanzibar na Nisiposema Mimi Nitawatuma Wasaidizi wangu Kuwaeleza" - Dk Shein


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema yeye bado ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na kutoa changamoto kwa wasioiamini Katiba hiyo kupeleka shauri hilo Mahakama Kuu ya Zanzibar ambayo ndiyo pekee yenye uwezo wa kutafsiri Katiba.

Amebainisha kuwa yeye anaongoza nchi kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwamba kama si uwezo huo aliopewa Kikatiba hana sababu ya kuendelea kukaa madarakani pamoja na serikali anayoingoza.

“Tuko madarakani na uongozi wote wa serikali… yupo Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili wa Rais na mawaziri” alisisitiza Dk. Shein na kuongeza kuwa hao wanaodai kujiondoa serikalini huo ni uamuzi wao wenyewe.

Alibainisha kuwa yeye na serikali anayoingoza kuendelea kuwepo madarakani “si uamuzi wake” na wala yeye hana “ubavu” wa kujiweka madarakani bali ni Katiba ambayo inajieleza wazi.

Dk. Shein ametoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu kisiwani humu kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.

Aliwaambia wananchi hao kuwa yako mengi yanayosemwa lakini hawapaswi kuyasikiliza kwa kuwa kama ni serikali yeye ndiye Rais hivyo wanapaswa kumuamini anachowaeleza.

“Ya mjini yapo yasikilizeni lakini kwa Serikali mimi ndiye Rais na nisiposema mimi nitawatuma wasaidizi wangu kuwaeleza” Dk. Shein alibaisha na kuongeza kuwa ya vyama kila mtu ana chama chake.

Alifafanua kuwa kama ni suala la Chama cha Mapinduzi (CCM) yeye ndiye Makamu Mwenyekiti Zanzibar na kama kuna la kuwaeleza wana CCM na wananchi atawaeleza yeye na viongozi wenzake wa chama hicho pamoja na taarifa za vikao vya chama vyake.

Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ushindani wa kisiasa si ugomvi bali ni utaratibu wa kupeana changamoto katika uongozi ambao lengo ni kuwaletea wananchi maendeleo.
 
“tusikejeli maendeleo yetu, tuthamini chetu na ushindani wetu wa kisiasa usirejeshe nyuma maendeleo yetu” Dk. Shein alitahadharisha.

Dk. Shein aliruejea wito wake wa kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yameanza tarehe 3 Januari na yanatarajiwa kufikia kilele tarehe 12 Januari, 2016 katika kiwanja cha Amaan.

Aliwakumbusha wananchi hao kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yaliyomfanya Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume kutangaza Jamhuri ya Zanzibar, ndiyo yaliyowakomboa wanyonge wa Visiwa vya Zanzibar kwa kuondosha aina zote za ubaguzi na kuwapa mamlaka ya kujiamulia mambo yao.

Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Pemba kuwa meli mpya iliyonunuliwa na Serikali MV Mapinduzi II ambayo ilizinduliwa hivi karibuni, itawasili kisiwani humo tarehe 10 Janauri na siku itakayofuata itawachukua baadhi ya wananchi kwenda Unguja kushiriki maaadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.

Alisisitiza kuwa serikali itawalipia gharama za usafiri wa kwenda na kurudi Unguja wale wote watakaoteuliwa kuwemo kwenye safari hiyo kufuatana na utaratibu utakaowekwa kama alivyokuwa ameahidi wakati meli hiyo ilipokuwa inatengenezwa nchini Korea ya Kusini.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Rais amefuatana na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na wabunge.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
E-mail:saidameir@ikuluzanzibar.go.tz& sjka1960@hotmail.com

No comments: