Siku
moja baada ya kuahirishwa ziara ya aliyekuwa mgombea urais kupitia
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, chama hicho
kimesema hakilitambui zuio la kufanya maandamano na mikutano ya kisiasa
lililowahi kutolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP)
Ernest Mangu mwezi uliopita.
Kauli
ya Chadema ilitolewa jana na Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini
Makene, baada ya kuulizwa juu ya kuwapo taarifa kuwa wameshindwa
kuendelea na ziara ya Lowassa kutokana na zuio hilo.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, baada ya kuahirishwa mkutano na waandishi wa
habari, Makene alisema katazo hilo la mikutano ya hadhara linaendelea.
“Hatulitambui
tamko la IGP, sisi tuliahirisha kutokana na kutingwa na shughuli za
uchaguzi mdogo, hivyo tukimaliza kushughulikia masuala hayo ya uchaguzi,
tutarudi kuendelea na ziara kama tulivyopanga nchi nzima. Hata kama IGP
kakataza, mbona CCM wanafanya mikutano ya hadhara?” alisema Makene.
Akizungumzia
sababu za kuahirisha mkutano ambao chama hicho kiliuitisha jana na
kusababisha waandishi wa habari kusubiri kwa zaidi ya saa tatu, Makene
alisema kuna masuala ya msingi ambayo yalijitokeza katika suala la umeya
wa Jiji la Dar Salaam ambalo ndilo lilikuwa ajenda.
“Tumeahirisha kwa sababu kuna figisufigisu tumefanyiwa kwenye umeya, hivyo tunazifanyia kazi,” alisema Makene.
Alisema
lengo la kuita waandishi wa habari ilikuwa ni kutangaza jina la mgombea
wa nafasi hiyo ya umeya wa Jiji la Dar es Salaam.
Mkutano
wa viongozi hao ulikuwa ukiendelea ndani ya ofisi za chama hicho, huku
kila mara baadhi ya viongozi wakitoka na kutoa matumaini kwa waandishi
kuwa mkutano wao utaanza punde.
Mwezi
uliopita, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake Advera Bulimba, lilipiga
marufuku maandamano na mikutano kutokana na kudai kuwa tathimini
iliyofanyika ilionyesha bado kuna mihemuko ya kisiasa ambayo
itasababisha uvunjifu wa amani.
No comments:
Post a Comment