MKUU
wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (pichani) ameamuru kusitishwa mara
moja malipo yanayofanywa kwa makandarasi waliojenga barabara tano za
ndani ya wilaya hiyo.
Amefanya
hivyo kwa maelezo kuwa watendaji wa Manispaa hiyo, wameshirikiana na
makandarasi hao kuiibia serikali Sh bilioni 5.7. Fedha hizo ni ongezeko
ambalo makandarasi hao, wanatakiwa kulipwa baada ya kujenga barabara
hizo, ambazo thamani halisi ya ujenzi huo ni Sh bilioni tano.
Lakini,
katika hali isiyo ya kawaida, makandarasi hao wanatakiwa kulipwa Sh
bilioni 10, ongezeko ambalo ni zaidi ya asilimia 100.
Akizungumza
jana Dar es Salaam, Makonda alisema taratibu za Serikali zinataka kama
barabara haikukamilika ndani ya muda uliowekwa kwa sababu mbalimbali,
ikiwemo mvua na sababu zinginezo, mkandarasi anatakiwa kulipwa fedha
zaidi ambazo ni asilimia 15 ya thamani ya fedha za mradi.
“Lakini
kinachostaajabisha katika miradi hii ya barabara, fedha ambazo
zimeongezeka ni zaidi ya asilimia 15, kiasi hiki ni zaidi pia ya
asilimia 100, wametumia utaratibu gani kulipa fedha hizi za ziada kwa
makandarasi hawa?” Alihoji Makonda.
Alizitaja
barabara ambazo watendaji wamezitumia kufisadi fedha za umma kuwa ni
ujenzi wa barabara ya Lion kwa kiwango cha lami yenye thamani ya Sh
milioni 592.1, lakini nyongeza ya fedha zilizoongezeka ni Sh milioni
860.1 na hivyo kufanya mradi huo kugharimu Sh bilioni 1.4.
Barabara
ya kutoka Biafra hadi Embassy, matengenezo yalikuwa ni Sh milioni 507.9
na fedha zilizoongezeka ni Sh milioni 487.5 jumla ya malipo kwa
mkandarasi ni Sh milioni 994, barabara ya Mabatini thamani ya mradi
ilikuwa Sh milioni 655.5 na fedha zilizoongezeka ni Sh milioni 777.8 na
jumla ya mradi kugharimu Sh bilioni 1.4.
Makonda
alitaja barabara nyingine zilizojengwa kwa kiwango cha lami zenye
ufisadi ni ya Journalism, ambayo ujenzi wake ulikuwa ugharimu Sh bilioni
mbili, nyongeza ya fedha katika mradi huo ni Sh bilioni 1.8 na hiyo
kufanya mradi huo hugharimu Sh bilioni 3.8, Barabara ya Maandazi ambayo
thamani ya mradi ni Sh milioni 799 imeongezwa kiasi cha fedha Sh bilioni
1.2 na hivyo kufanya mradi wote kugharimu Sh bilioni 2.
“Nyongeza
hizi zinatia shaka na ni jambo la kushangaza, nimeamuru makandarasi
wasiendelee kulipwa fedha hizi na nimetoa siku tano kwa ofisi ya
uchunguzi ya mkoa ichunguze malipo haya na mafaili ya miradi hiyo
yaletwe ofisini kwangu mara moja,” alisema Makonda.
Alisema ili malipo ya ziada yalipwe, lazima Bodi ya Zabuni ya Wilaya na Bodi ya Mfuko wa Barabara, ziidhinishe malipo hayo.
“Lakini
cha kushangaza katika malipo haya, yanayoendelea kufanywa na Manispaa,
makandarasi wamelipwa kabla hata bodi hazijatoa ukubali wa malipo haya
kufanyika,” alisema.
Alisema
Bodi ya Mfuko wa Barabara katika ripoti yao, walikataa fedha hizo za
malipo ya zaida zisitolewe. Lakini, alisema fedha hizo zilitolewa na
Manispaa kwa makandarasi hao na hiyo inaonesha kwamba kuna mchezo
mchafu, umefanywa kati ya watumishi wa Manispaa na makarandasi wenyewe.
Alisema
wahusika wakuu katika malipo hayo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa,
Kitengo cha Manunuzi, Mhandisi wa Barabara wa Manispaa ambao ndio
wanatakiwa kutoa maelezo ya kuwepo kwa nyongeza hiyo ya malipo kinyume
cha taratibu za Serikali.
“Watu
wanadai naingilia kazi za watu, nisipobaini uozo huu kwenye wilaya
yangu sifai kuwa mkuu wa wilaya, haiwezekani watu wafisadi fedha za umma
kiasi hiki wakati tunakosa hata pesa ya kujenga wodi ya wazazi pale
Hospitali ya Mwananyamala,” alisema Makonda.
Alisema
ataendelea kupambana, kuhakikisha kwamba kila mwananchi anafaidika na
keki ya Serikali ;na sio watu wachache ambao wamepewa dhamana ya kufanya
kazi kwenye ofisi za umma wafaidike na keki hiyo.
Barabara
hizo ni nje ya barabara zingine, ambazo Makonda mwanzoni mwa mwaka huu
aliziundia tume kuchunguza ujenzi wake, ambao walidai ulikuwa chini ya
kiwango hali inayofanya mvua zikinyesha barabara hizo zinageuka
mahandaki.
Tume hiyo ilibaini ujenzi kuwa chini ya kiwango, lakini mabilioni ya fedha zimetumika katika ujenzi huo.
Ilipendekeza hatua kuchukuliwa kwa wahusika waliohusika kujenga barabara hizo, ambazo mvua ikinyesha zinageuka mashimo.
No comments:
Post a Comment