Yanga Yatangaza Kuvunja Mkataba Na Haruna Niyonzima....Yamtaka Kulipa Fidia ya Dola 71,175 - LEKULE

Breaking

28 Dec 2015

Yanga Yatangaza Kuvunja Mkataba Na Haruna Niyonzima....Yamtaka Kulipa Fidia ya Dola 71,175

Afisa Habari wa klabu ya Yanga Jerry Muro wakati akizungumza na waandishi wa habari leo makao makuu ya klabu ya Yanga juu ya kuvunjwa mkataba kati ya klabu ya Yanga na Haruna Niyonzima
*********
Klaubu ya Yanga imetangaza kuvunja mkataba na kiungo wake wa kimataifa kutoka nchini Rwanda Haruna Niyonzima kutokana na utovu wa nidhamu ikiwemo kuchelewa kuripoti kambini na kutoipa kipaumbele klabu yake.

Nahodha huyo wa Rwanda alichelewa kurejea kwenye klabu yake mara baada ya kumalizika kwa fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CEFAFA Challenge Cup) iliyofanyika nchini Ethiopia.

Niyonzima ambaye alikuwa akikitumikia kikosi cha timu yake ya taifa aliwasili Dar es Salaam December 16 mwaka huu wakati michuano ya Challenge Cup ilimalizika December 6.

Baada ya kuwasili Niyonzima alitoa utetezi wake kwamba alikuwa akisumbuliwa na majeraha aliyoyapata kwenye michuano ya Challenge kwani alikuwa amefungwa bandage ngumu mguuni. Lakini Yanga ilihitaji uthibitisho wa ripoti ya daktari wake wa timu ya taifa.

December 17, Yanga ilitoa adhabu ya kumsimamisha mchezaji huyo kwa muda usiojulikana huku akiendelea kupokea nusu mshahara kwa muda wote huo aliosimamishwa kwa kipindi kisichojulikana.
Adhabu hiyo ilitangazwa na Katibu mkuu wa Yanga Dkt. Jonas Tiboroha baada ya kamati ya mashindano kuazimia adhabu hiyo iwe ni ya awali wakati ikiendelea kujadili ni adhabu gani stahiki itolewe kwa Niyonzima ambaye amejijengea umaarufu mkubwa kwenye soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.


Leo afisa habari wa Yanga Jerry Muro ametangaza uamuzi uliofikiwa na klabu ya Yanga wa kuvunja mkataba na Niyonzima huku ikimtaka Niyonzima ailipe klabu hiyo zaidi ya dola za kimarekani 71,175 kama fidia inayotokana na mkataba mpya unaomalizika mwaka 2017.

No comments: