Wenyeviti wa CCM Mikoa Wampongeza Rais Magufuli Kwa Kasi Aliyoanza Nayo - LEKULE

Breaking

7 Dec 2015

Wenyeviti wa CCM Mikoa Wampongeza Rais Magufuli Kwa Kasi Aliyoanza Nayo


WENYEVITI wa Mikoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini, wamempongeza na kuunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Rais John Magufuli za kutumbua majipu. 
 
Wamempongeza Dk Magufuli kwa hatua za kubana matumizi ya umma, kuziba mianya ya rushwa, kupiga vita ubadhirifu wa mali ya umma na kurejesha nidhamu na uwajibikaji kwenye taasisi za umma na nchi kwa ujumla.

Aidha, wenyeviti hao kwa pamoja wanamuombea kiongozi huyo na wasaidizi wake wote afya njema na hekima itokayo kwa Mwenyezi Mungu katika kutekeleza kazi zao kwa wepesi na kasi ili kuleta maendeleo endelevu, kukuza umoja wa kitaifa na kuimarisha mustakabali wa nchi na watu wake.

Katika taarifa yao ya kupongeza ushindi kwa Dk Magufuli na Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu katika uchaguzi uliomalizika Oktoba mwaka huu, wenyeviti hao walisema wanaungana bega kwa bega na viongozi hao katika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2015/2020.

“Tunamwomba Rais Magufuli aendeleze kasi yake ya kutekeleza majukumu yake na asisite kuwawajibisha watendaji wote wazembe wanaozalisha kero ya utoaji huduma duni kwa wananchi. 
 
"Sisi tutazidi kuungana naye katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye mikoa yetu na kuzihimiza ngazi zote za uongozi wa chama kufanya hivyo bila kusababisha mwingiliano wa kimajukumu,” alisema Mwenyekiti wa Wenyeviti hao, Ramadhani Madabida wakati akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam.

Madabida alisema pia wanampongeza Dk Magufuli kwa uteuzi alioufanya hivi karibuni wa nafasi ya Waziri Mkuu kwa kumteua Kassim Majaliwa kushika wadhifa huo.
 
 Alisema uteuzi huo umeonesha mwelekeo wa aina ya Baraza la Mawaziri analotegemea kuliunda na hazina kubwa ya viongozi wachapakazi na wanyenyekevu na watumishi bora wa umma waliopo ndani ya CCM.

“Tutakuwa hatukumtendea haki, kama tutaacha kumpongeza Rais kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa kwenye ufunguzi wa Bunge la 11, hotuba ile ni mwongozo na mwelekeo wa Tanzania tunayoitarajia, na imehuisha matumaini ya Watanzania na kuleta ari ya uzalendo na haja ya kulitumikia taifa lao,” alisema Madabida ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Pamoja na hayo, wenyeviti hao wamefadhaishwa na vitendo vya ukosefu wa nidhamu, vilivyofanywa na wabunge wa kambi ya Upinzani vya kupiga kelele na kusababisha kutolewa nje kabla ya Dk Magufuli kutoa hotuba yake.

“CCM inazitaka mamlaka zinazoendesha vyombo vya Bunge na Baraza la wawakilishi kuchukua hatua stahiki kukomesha vitendo kama hivyo kwa vile vinadumaza demokrasia. Tunawaasa Waheshimiwa Wabunge kuwa mfano wa mwenendo bora na desturi za jamii wanayoiongoza,” ilisisitiza.

Viongozi hao walimpongeza Dk Magufuli na Suluhu kwa ushindi walioupata katika uchaguzi huo na kuwashukuru wanaCCM na wananchi kwa ujumla kwa kukipigania chama hicho na kukirejesha tena madarakani.

Madabida alisema katika kampeni zilizoendeshwa kote nchini, Dk Magufuli aliahidi Watanzania watakapomchagua kuwa Rais atatekeleza kwa juhudi na maarifa masuala ya kuondoa umasikini; kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana; kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma na kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama kwa maisha ya wananchi na mali zao.


“Alisisitiza kutowaangusha Watanzania kwa kaulimbiu yake isemayo “Hapa Kazi Tu,” alisema Madabida na kusisitiza kuwa tayari ahadi hizo zimeanza kutekelezwa kwa vitendo vinavyoonekana.

No comments: