Watumishi Waandamizi 7 wa TANESCO Wafukuzwa kazi kwa Tuhuma Mbalimbali - LEKULE

Breaking

6 Dec 2015

Watumishi Waandamizi 7 wa TANESCO Wafukuzwa kazi kwa Tuhuma Mbalimbali


UFAFANUZI WA MASUALA MBALI KWA WATEJA WA TANESCO KUPITIA VYOMBO VYA HABARI.

 
1. HALI YA UZALISHAJI UMEME NCHINI

Hali ya umeme nchini imeendelea kuimarika licha ya changamoto mbali mbali tunazokabiliana nazo kwa sasa. Kuanzia taerehe 17 Septemba tulipoanza kutumia gesi inayotoka Mtwara tumeweza kuongeza uzalishaji wa umeme unaotumia gesi kutoka Megawati 260 zilizokuwepo kabla hadi Megawati 560 ikiwa ni ongezeko la jumla ya Megawati 300 au asilimia 115 ya umeme wa gesi uliokuwa unazalishwa. Hii imechangia sana kuboresha hali ya umeme tofauti na ilivyokuwa hapo kabla. 


Tunategemea kuongeza umeme wa Megawati 130 zaidi kutokana na vyanzo vya Gesi kati ya sasa na mwishoni mwa mwezi Januari 2016. Hii itafanya jumla ya umeme wote unaotokana na gesi kufikia Megawati 700 sawa na asilimia 70 ya umeme wote kwenye Gridi ya Taifa.

Haya ni mapinduzi makubwa kwani kwa miaka mingi vyanzo vya maji ndivyo vimekuwa vikichangia zaidi ya asilimia 70 ya umeme nchini na hivyo kusababisha athari za mara kwa mara kila unapotokea ukame.
 
Pamoja na hayo yaliyokwishafanyika, Mkandarasi wa mradi wa pili wa Kinyerezi (KII) wa Megawati 240 anatarajia kuanza kazi wakati wo wote kuanzia sasa baada ya kuwa amekwishalipwa sehemu ya fedha za awali za kuanza kazi hiyo.
 

2. MIUNDOMBINU YA TANESCO

Miongoni mwa kero kubwa inayolalamikiwa sana na wateja wetu ni kukatika umeme kunakosababishwa na uchakavu wa miundombinu. Ukweli ni kwamba baadhi ya miundombinu tuliyo nayo ni ya siku nyingi wakati matumizi ya umeme
yameendelea kuongezeka kwa kasi sana.

Kwa mfano nyingi ya Substations katika jiji la Dar es Salaam zimejengwa katika miaka ya 80 na 90. Wakati huo wakazi wa jiji la Dar es Salaam walikuwa chini ya milioni 3. Sasa hivi wakazi wa jiji ni zaidi ya milioni 5 na hivyo miundombinu iliyopo inaelemewa sana.
 
Jitihada za kurekebisha hali hii zilikwishaanza ambapo sasa kuna miradi mikubwa inaendelea katika jiji la Dar es Salaam na itakapokamilika itasaidia sana kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme. Kwa kiasi fulani kukatika huko kwa umeme hasa katika jiji la Dar es Salaam kunatokana pia na utekelezaji wa miradi hiyo.
 
Miradi inayotekelezwa ni pamoja na ule unaojengwa kusini mwa Dar es Salaam kwa mkopo wa Benki ya Dunia ambao utaboresha umeme maeneo ya Kigamboni, Kurasini, Mbagala, Mkuranga, Kisarawe, Gongolamboto, Ukonga, Kitunda, Vingunguti na Tabata
 
Mradi mwingine ni unaotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan ambao utasaidia kuondoa matatizo yaliyo katika maeneo ya Muhimbili na Upanga, Mwananyamala na Kinondoni, Oysterbay na Masaki, Jangwani Beach, Bahari Beach na Mbezi Beach.
 
Mradi mwingine ni ule unaotekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ambao unaendelea katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Shinyanga, na Geita.
 
Mradi mwingine ni ule unaofadhiliwa na Serikali ya Finland ambao utasaidia sana kuimarisha umeme kati kati ya jiji la Dar es Salaam na kusaidia kuimarisha umeme katika eneo lenye majengo mengi marefu la Samora, Azikiwe, Kariakoo na Sea view.
 
Sambamba na miradi hiyo inayotekelezwa Dar es Salaam, mradi mkubwa wa kupeleka umeme wa 400KV kutoka Iringa kupitia Mtera, Dodoma, Singida hadi Shinyanga uko kwenye hatua za mwisho za kukamilika na hivyo kutuhakikishia umeme wa uhakika katika kanda ya ziwa hasa jiji la Mwanza.
Kazi ya kuunga Songea na Gridi ya Taifa kutokea Makambako kwa 220KV inaendelea na Makandarasi wako kazini.
 
Kazi za kuunga Tanzania na Kenya kwa umeme wa 400KV inatarajiwa kuanza hivi karibuni kwani zabuni za kuwapata Makandarasi ziko katika hatua za mwisho. Ujenzi unategemewa kuanza mwakani.
 
Kazi nyingine ambazo hazijaanza lakini zitaanza hivi karibuni ni pamoja na Dar es Salaam – Somanga (400KV), Bulyankhulu – Geita – Nyakanazi – Rusumo (220KV)
 
Miradi hii ya kuimarisha miundombinu ikikamilika itasaidia kulipunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la kukatika kwa umeme kutokana na mfumo wa Usambazaji.
 
Nawaomba wateja wetu, wakati kazi hii kubwa inapoendelea, wawe na subira na uvumilivu kwa usumbufu wa hapa na pale utakaokuwa unatokea. Hata hivyo TANESCO itajitahidi kurekebisha kasoro zinazoweza kurekebishwa katika miundombinu ya sasa ili kupunguza usumbufu huo wakati marekebisho makubwa yakiendelea.

 
3. KERO ZA HUDUMA KWA WATEJA

Ukiacha kero zinazosababishwa na Miundombinu, TANESCO inachukua hatua madhubuti za kuwaadibisha wafanyakazi
wake wanaotoa huduma mbaya na kuwa kero kwa wateja. Baadhi ya kero ambazo zimekuwa zikilalamikiwa ni pamoja na lugha mbaya, wateja kudaiwa rushwa kabla ya kupewa huduma, kucheleweshewa huduma, ubadhirifu nk.
 
Shirika linapenda kuwahakikishia wateja wake kuwa tayari limeshaanza kuchukua hatua kali kwa wafanyakazi wanaobainika kujihusisha na mambo hayo. Kwa mfano katika kipindi cha miezi miwili Shirika limewaachisha kazi maofisa 7 waandamizi kutokana na makosa mbali mbali ikiwemo wizi na ubadhirifu. 

Miongoni mwao ni wale waliofikishwa mahakamani kule Kagera na kuripotiwa na vyombo vya habari jana. Walioachishwa kazi ni pamoja na wafanyakazi wa ngazi za Mameneja, Wahandisi na Wahasibu.
 
Shirika litaimarisha hatua hizo ambapo mfanyakazi ye yote atakayebainika analaghai wateja, anadai rushwa, anatoa lugha chafu au huduma mbovu atawajibishwa mara moja na pale atakabobainika kuachishwa kazi.
 
Tumeanza maandalizi ya kutoa namba maalum za simu kwa wateja wetu ambazo zitatumika kutoa taarifa ya vitendo kama hivyo vinavyofanywa na wafanyakazi wetu ili hatua muafaka ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

 
4. KUDHIBITI WIZI WA UMEME

Shirika linaendelea na Kampeni maalum katika mikoa yote ya kuwakamata wezi wa umeme na kuwachukulia hatua kali. Pamoja na hatua nyingine zitakazochukuliwa, wezi wa umeme watakuwa wanatangazwa hadharani na kufunguliwa mashtaka. 

Hivyo ninatoa rai kwa ye yote ambaye amekuwa akijihususha na wizi wa umeme ajisalimishe mwenyewe kwa kwenda kwa Meneja wa Mkoa anakopatia huduma. Kama
hawatajisalimisha kwa hiari hatua zilizokusudiwa dhidi yao zitachukuliwa pasipo huruma yo yote.
 
Tunatoa siku saba kwa wateja wanaojua kwamba mita zao zimechezewa kujisalimisha wao wenyewe la sivyo TANESCO haitalaumiwa kwa hatua tutakazochukua.

 
5. UNUNUZI WA NGUZO KUTOKA KWA WAZALISHAJI WA NDANI

Tunapenda kufafanua kwamba Wazalishaji nguzo wa ndani ya nchi wana nafasi sawa ya kuuza nguzo zao TANESCO kwa mujibu wa sheria ya manunuzi. 

Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vilidai kwamba TANESCO inakusudia kununua nguzo 700,000 kutoka Afrika Kusini kwa dola za Marekani 115 milioni! Taarifa hizo ni za uongo na uzushi wa hali ya juu. 

Kwa mfano; TANESCO itawezaje kununua nguzo kwa dola miliomi 115! Hizo ni fedha nyingi mno ambazo huenda zingetosha kuwekeza Mtambo mpya wa umeme wa zaidi ya Megawati 100. Itazipata wapi fedha hizo kwa ajili ya kununua nguzo tu?
 
Ukweli ni kwamba tuna wasambazaji kadhaa wa nguzo kutoka ndani ya nchi na wengine kutoka nje. Wote hupatikana kwa ushindani kulingana na Sheria ya Manunuzi. Vigezo vinavyozingatiwa ni Ubora wa nguzo zao na bei.
 
Baadhi yao waliwahi kupata zabuni lakini wakashindwa kuleta nguzo ikabiidi zabuni ile ivunjwe na Waziri, baadhi yao ililazimu kuwanyang’anya zabuni na kuwapa wa nje baada ya kushindwa kusambaza nguzo na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wateja.

 
6. USHIRIKI WA TANESCO KWENYE ZOEZI LA USAFI TAREHE 9 DESEMBA 2015

Wafanyakazi wote wa TANESCO watashiriki katika shughuli mbali mbali za usafi wa mazingira katika maeneo yote yanayozunguka ofisi, mitambo na vituo vyetu nchi nzima. Hii inaenda sambamba na agizo la Mh. Rais la kuitumia siku ya tarehe 9 Desemba kwa ajili ya shughuli za usafi. 

Hii itahusisha pia usafi kwenye substations, kando kando ya Transforma na maaeneo mengine yenye miundombinu yetu. Tayari maandalizi ya kazi hizo yamekwishaanza na tutashiriki kikamilifu.
 
Ahsanteni kwa kunisikiliza

No comments: