WANAFUNZI WALIOWAHI KUSOMA ENABOISHU KUKUTANA KUPANGA MIKAKATI YA KUSAIDIA SHULE YAO - LEKULE

Breaking

4 Dec 2015

WANAFUNZI WALIOWAHI KUSOMA ENABOISHU KUKUTANA KUPANGA MIKAKATI YA KUSAIDIA SHULE YAO

Na Zawadi Msalla-MAELEZO
WANAFUNZI waliowahi kusoma katika shule ya Sekondari Enaboishu ya jijini Arusha wanatarajia kukutana tarehe 5 Desemba 2015 ili kujadili masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuisaidia shule hiyo katika kuboresha maendeleo ya taaluma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Muda  wa Jumuiya hiyo ya Enaboishu Renalda Shirima alisema mkutano huo wa kwanza utafanyika katika matawi mawili ya mkoa wa Arusha na Dar es salaam. 

Ambapo katika mkoa wa Dar es salaam utafanyika katika ukumbi wa Triple Seven eneo la Kawe  na Arusha katika club ya AICC Kijenge. 

Renalda alisema jumuiya hiyo ina malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuangalia fursa mbalimbali ambazo wanaweza kushirikiana katika kuleta maendeleo ya taaluma katika shule yao ya zamani kwa kuboresha mazingira ya wanafunzi na walimu ya kujifunzia na kufundishia.

“Tutaweza kufahamiana kwa karibu zaidi kwa watakao hudhuria na pia kupata mawasiliano ya wale ambao hawata hudhuria, hii pekee ni chachu ya kuleta maendeleo” alisema Renalda.

Aliongeza kuwa kwa sasa zipo changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu ambazo kwa pamoja kama Taifa ni lazima kuungana ili kuweza kuisaidia Serikali katika kuzitatua. Jumuiya hiyo ya wana Enaboishu imedhamiria kwa dhati kulipa fadhila katika shule yao ili kuondoa changamoto hizo.

Aidha alisema wanatajaria kuweka mkakati wa kuishauri Serikali namna ya kuwatumia wahitimu wa zamani wa shule mbalimbali nchini ili kuboresha miundombinu ya shule walizo soma.
“Tungependa utamaduni huu sasa ujengeke na uenee nchi nzima” Alisema.

Mwenyekiti huyo wa muda alisema katika kikao hicho pia wanatarajia kuchagua uongozi wa kudumu  wa umoja huo.


Shule ya Sekondari ya Enaboishu imeanzishwa mwaka 1966. Mpaka sasa shule hiyo imeshatoa wahitimu ambao wako katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani na nje ya nchi. Baadhi ya viongozi wakubwa walio wahi kusoma katika shule hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel. 

No comments: