Serikali ya Ujerumani imeeleza kufurahishwa na kasi ya kupambana na rushwa na ufisadi ya Rais John Magufuli na kuahidi kumpa ushirikiano katika masuala ya maendeleo.
Ujerumani
inakuwa nchi ya kwanza ya kigeni kuvutiwa na kasi ya Rais Magufuli
ambaye ameonekana kuelekeza nguvu katika si tu kupambana na maovu hayo
tangu aapishwe Novemba 5, bali pia kuchochea maendeleo ya watu wenye
kipato cha chini.
Aidha,
Ujerumani imesema inasubiri kuona vipaumbele vya maendeleo
vitakavyoainishwa na serikali ya Rais Magufuli ili iweze kuisaidia
utekelezaji.
Pongezi hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Georg Schmidt.
Akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu ziara yake ya siku tano hapa nchini,
Schmidt alisema katika kipindi cha mwezi mmoja tu, Dk. Magufuli ameweza
kushughulikia masuala muhimu ya kijamii ikiwamo kuboresha huduma za afya
na kuwashughulikia wakwepa kodi.
Kasi
ya Rais Magufuli, alisema, itasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo
zitakapokusanywa zitachangia miradi mbalimbali ya maendeleo kama
alivyofanya tayari kwenye afya na elimu.
Mkurugenzi
huyo alisema ziara yake nchini ilikuwa na lengo la kuangalia hali ya
maendeleo nchini baada ya uchaguzi, miradi ya maendeleo inayotekelezwa
na serikali yake pamoja na kukuza ushirikiano baina ya nchi mbili hizo.
Alisema
ameshakutana na baadhi ya watendaji wa serikali, wabunge, wanaharakati,
watendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kuitembelea Mahakama
ya Haki za Binadamu iliyopo mjini Arusha.
Alisema
pia amekuja kuangalia fursa za kibiashara nchini kwa sababu wawekezaji
wengi duniani huvutiwa kwenda kuwekeza kwenye mataifa mbalimbali iwapo
nchi hiyo ina usalama wa kutosha.
Akizungumzia
suala la Zanzibar, Schmidt aliwataka wananchi kuwa na subira wakati
mazungumzo yakiendelea katika jitihada za kutatua mgogoro huo.
“Mazungumzo yanaendelea ya usuluhishi tunasisitiza utulivu, amani na tuna imani mwafaka mzuri utafikiwa,” alisema.
Alisema
kwa sasa serikali ya Ujerumani itazielekeza fedha nyingi kwa serikali
ya Tanzania ili kushughulikia wakimbizi kutoka Burundi wanaokimbia
machafuko.
“Tuna
jukumu na wajibu wa kushughulikia mgogoro wa Burundi na fedha
zilizokuwa zinakwenda Burundi sasa zitaelekezwa Tanzania kwa kuwa
wanapokea wakimbizi wengi zaidi,” alisema Schmidt.
No comments:
Post a Comment