Spika wa Bunge, Job Ndugai ni mgonjwa na yupo India kwa matibabu.
Katibu
wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema jana kuwa Ndugai yuko nje ya
nchi kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake bila ya kusema amekwenda nchi
gani wala ugonjwa unaomsumbua.
“Ni
kweli Spika yupo nje, lakini alikwenda kwa ajili ya kufanya uchunguzi
tu, siyo kwamba anaumwa sana, hapana ila hii ni mara ya pili kwenda
kufanya uchunguzi huo. Hata ukitaka kuzungumza naye mpigie simu
mtazungumza naye maana hali yake inaendelea vizuri na yuko salama,” alisema Dk Kashilila.
Balozi wa Tanzania nchini India, John Kijazi alipopigiwa simu ili kujua kama kiongozi huyo yuko huko, alisema:
“Ni kweli yuko hapa India kwa matibabu na anaendelea vizuri. Unaweza kumpigia wewe mwenyewe uzungumze naye.” Alisema Kijazi bila kuweka wazi kwamba yuko hospitali gani na nini hasa kinachomsumbua.
Ndugai
hajaonekana hadharani, kwa muda mrefu, hata katika shughuli muhimu za
kitaifa ambazo zimekuwa zikifanywa na Rais John Magufuli, hivyo kuacha
maswali mengi kutoka kwa wananchi.
Shughuli
mojawapo ambayo Spika huyo hakuhudhuria ni ile ya kuapishwa mawaziri
wapya Jumamosi iliyopita Ikulu, Dar es Salaam. Naibu Spika, Dk Tulia
Akson ndiye alihudhuria.
No comments:
Post a Comment