KAMPUNI
ya serikali inayotoa huduma za meli katika eneo la Maziwa Makuu, Marine
Services Company Ltd (MSCL), inadaiwa kutumia kinyume sh.milioni 300
kati ya milioni 600 ilizokuwa imepewa kutengeneza meli ya Mv.Victoria.
Hali
hiyo iligunduliwa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mwanza Magesa Mulongo baada
ya kutembelea ofisi za kampuni hiyo zilizopo Bandari ya Mwanza
Kaskazini.
Uongozi
wa MSCL unadaiwa kutumia fedha hizo kulipa mishahara badala ya
kutengeneza meli hiyo iliyojengwa mwaka 1964, ambayo kwa zaidi ya mwaka
mmoja sasa imeegeshwa katika Bandari ya Mwanza Kusini, kutokana na
kuharibika kwa baadhi ya mitambo na kangavuke (Generator) ya kufua
nishati ya umeme melini.
Hali hiyo imewaathiri vibaya abiria na wasafirishaji wa mizigo kati ya Mwanza na Bukoba.
Desemba
mwaka jana Mv Victoria ilipandishwa kwenye chelezo ili ifanyiwe
matengenezo,kazi iliyopaswa kuanza Julai mwaka huu, lakini haikufanyika
kutokana na fedha kukosekana; hivyo ikashushwa kutoka kwenye chelezo.
Imedaiwa
kuwa matengenezo ya meli hiyo inayotegemewa na wakazi wa Mikoa ya
Mwanza na Kagera,yamekwama kutokana na kiasi cha fedha kutumika kulipa
mishahara ya wafanyakazi na kiasi kingine kununua vipuri kwa ajili ya
kufanyia ukarabati wa meli nyingine (Mv.Serengeti) kinyume na maelekezo
ya serikali.
Mkuu wa mkoa autuhumu uongozi
RC
Mulongo alisema kitendo cha uongozi kujichukulia uamuzi wa kumega kiasi
cha fedha hizo bila utaratibu,kimesababisha wananchi wanaosafiri na
kusafirisha mizigo yao kati ya Mwanza na Bukoba kwa kutumia meli hiyo,
kukosa huduma hiyo sababu ya watu wachache kutofuata taratibu za
matumizi ya fedha za umma.
Alisema
kama fedha hazikutolewa zote,ilipaswa ifanyiwe matengenezo ya awali
wakati mambo mengine ya mishahara yao yakiendelea kushughulikiwa.
"Lakini
ninyi mmejimegea chenu kwa madai meli hazifanyi kazi,menejimenti ya
kampuni hii imekosa mipango na mikakati na vipaumbele vya kusaidia
kubuni na kufufua meli hiyo. Hata kama fedha zitatolewa ni kazi bure," alisema Mulongo.
Kampuni yanena
Mhasibu
Mkuu wa MSCL, Beatus Rugarabamu na Kaimu Mrakibu wa Meli, Exavery
Kapinga, walisema sababu ya kuchukua kiasi cha fedha hizo na kulipana
mishahara ni kuyumba kwa uendeshaji wa biashara kunakotokana na kusimama
kwa meli karibu zote za kampuni hiyo, isipokuwa mbili tu, kwa sababu ya
uchakavu.
Kapinga
alisema kampuni hiyo ya huduma za meli za usafirishaji abiria na mizigo
iliyoanzishwa mwaka 2009,ina jumla ya meli 14, kati ya hizo tisa zikiwa
kwenye Ziwa Victoria, tatu Ziwa Tanganyika na mbili ziko Ziwa Nyasa.
Kapinga
alisema kati ya meli zote hizo, ni mbili tu zinazofanya kazi tena kwa
kusuasua ambazo ni Mv Serengeti ya Ziwa Victoria na nyingine iliyopo
Ziwa Nyasa.
Alisema
ili meli hizo ziweze kutengemaa na kufanya kazi zinahitajika sh.
bilioni 8.93 kwa ajili ya matengenezo, ndipo kampuni itapata uhai na
kuendelea kutoa huduma kwa faida.
No comments:
Post a Comment