SERIKALI YATAKA KILA KAYA KUWA NA CHOO BORA - LEKULE

Breaking

4 Dec 2015

SERIKALI YATAKA KILA KAYA KUWA NA CHOO BORA


SERIKALI imewaagiza maafisa  wa  afya nchini  kuhakikisha  kila kaya inakuwa  na choo bora  ikiwa ni hatua ya kuhakikisha  jamii inaepekana  na magonjwa  yanayotokana na uchafu  mazingira , sambamba  na   suala la usafi wa mazingira  kuwa endelevu  kama ilivyoagizwa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.  John Pombe Magufuli.
Aidha Serikali imepiga marufuku ulaji wa matunda yaliyomenywa barabarani.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Donan Mmbando(Pichani),wakati wa mkutano wake na  waandishi  wa habari  uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa  wizara hiyo.

Katibu Mkuu huyo ambaye alikuwa ameambatana na baadhi ya viongozi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu, wakiwemo wa wizara yake kwa ajili ya kuzungumzia mambo matatu ambayo ni  suala la usafi  wa mazingira  katika kuadhimisha siku ya  Uhuru ,Desemba 9, mwaka 2015, ugonjwa wa kipindupindu na  polio.
“Wakuu wa mikoa na wilaya wanatakiwa kutekeleza agizo hili kwa kujiwekea utaratibu wa kufanya usafi maeneo yao,” alisema Dkt. Mmbando.

 Dkt. Mmbando alisema  ikumbukwe kuwa ugonjwa wa kipindupindu pamoja na magonjwa mengine yanayohusiana na uchafu huenea kwa kasi kutokana na hali duni ya usafi katika maeneo tunayoishi. Hivyo takwimu zinaonesha kuwa kati ya taka ngumu zinazozalishwa ni 50% tu huzolewa na kupelekwa dampo. Kiasi cha taka kinachobaki huzagaa katika maeneo mbalimbali hususani kando kando ya barabara, katika maeneo ya kukusanyia taka (Collection points), chini ya madaraja na katika maeneo ya wazi hali inasayobabisha miji yetu kuonekana michafu. 

“Hali kadhalika, takwimu zinaonesha kuwa ni kaya zipatazo 34% ndizo zina vyoo bora na asilimia 12% hazina vyoo kabisa. Hali hii inahatarisha afya ya jamii na kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza.  Kwa mijini na miji midogo, mifereji ya maji taka na ile ya mvua ni michafu na mingi imeziba, hivyo hutiririsha maji ovyo na kuhatarisha afya ya jamii,” alisema .

Aliwataka watendaji hao, kusimimia suala hilo kwa kuzingatia sheria za afya  zilizopo, huku akizitaka halimashauri na mamlaka kuweka sheria ndogo ndogo ambazo hazileti unyanyasaji kwa wananchi. Katika kutekeleza kwa vitendo agizo la Mhe. Rais .

Kubainisha maeneo yote ya umma ambako shughuli za usafi wa mazingira zitafanyika siku hiyo,kuhamasisha jamii kwa njia mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki shughuli za usafi katika maeneo yao na sehemu za kazi au biashara, vyombo vya usafiri wa abiria na vituo vya wasafiri ili vifanyiwe usafi wa kuridhisha,kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi, vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za elimu, n.k. ili kufanikisha zoezi zima la ukusanyaji, usafirishaji na utupaji salama wa taka (madampo) kutoka katika maeneo ya kaya, umma na taasisi kwa siku hiyo.

Aliongeza kwamba  wanapaswa kuhusisha au kushirikisha vyombo vya habari vya kitaifa na kijamii katika kuhamasisha jamii kushiriki zoezi la usafi,kupanga ratiba na wajumbe wa kusimamia kazi hiyo katika halmashauri kwa tarehe 9,Desemba,2015  kwenye maeneo ya kaya na ya umma na kupanga ratiba endelevu baada ya hapo,kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa kazi hizi kwa mfumo na muda ulioinishwa na Wizara.

Pia kwa kushirikiana na wadau, halmashauri zina wajibu wa kuandaa vyombo vya usafirishaji taka ngumu na maji taka kutoka maeneo ya uzalishaji hadi maeneo yaliyoainishwa kutupwa bila kuathiri mazingira.
Kwa upande wa wananchi  aliwataka  wafanye yafuatayo ili  kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kila mmoja Kuchemsha maji ya kunywa au kutibu kwa dawa maalumu (waterguard)Kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salamaKunawa mikono kwa sabuni na maji safi na salama,kabla ya kula,baada ya kutoka chooni.

Mambo mengine ni baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia,baada ya kumhudumia mgonjwa,kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula,Kukomesha utiririshaji wa maji kutoka chooni ,Kutoa taarifa katika kituo cha kutolea huduma za afya endapo utapatwa na ugonjwa wa kuharisha au kutapika,kutoa taarifa kwenye ofisi za serikali endapo mtu au kikundi cha watu kitafanya shughuli zenye kuashiria uchafuzi wowote wa mazingira.

Aliongeza kwamba Serikali itaendeleza juhudi za kuwezesha wananchi kupata maji safi na salama. Napenda kusisitiza kwa wananchi wote, tuwe makini kutumia maji yanayotoka katika vyanzo visivyo salama. Hii ni muhimu kwani, kwa sehemu kubwa, ugonjwa huu huenezwa kupitia maji yasiyo salama.
Tangu kutokea kwa ugonjwa huu kwa mara ya kwanza tarehe 15 Agosti, 2015 katika mkoa wa Dar es Salaam ugonjwa huu umeendelea kusambaa kwa kasi. Hadi tarehe 2/12/2015 Mikoa mingine 20 ya Morogoro, Iringa, Pwani, Kilimanjaro, Kigoma, Dodoma, Geita, Mwanza, Arusha, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Tanga, Lindi, Rukwa, Manyara, Kagera, Katavi na Mbeya imeshaathiriwa.

 Takwimu zinaonesha kuwa hadi tarehe 2 Desemba, 2015 jumla ya watu 9,906 walipata ugonjwa  huu  na kati yao jumla ya watu 149 wameshafariki  dunia kutokana  na  ugonjwa huu. 

Aidha, wagonjwa wengine wamepata matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani ambapo hadi tarehe 2 Desemba, 2015 jumla ya wagonjwa 128 waliendelea kupatiwa matibabu katika vituo vya kutolea huduma

No comments: