Sadaka ya Mkesha wa Mwaka Mpya kuweka umeme Tabora - LEKULE

Breaking

30 Dec 2015

Sadaka ya Mkesha wa Mwaka Mpya kuweka umeme Tabora


Kanisa la ‘Tanzania Fellowship of Churches’ ambao ndio waandaaji wa mkesha mkubwa kitaifa wa mwaka mpya wa 2016 limeeleza kuwa fedha zitakazotokana na sadaka za siku hiyo zitaelekezwa kusaidia upatikanaji wa nishati ya umeme wa jua ya Solar Power katika hospitali mbalimbali za Tabora vijijini.

Mkesha huo utakaofanyika usiku wa Desemba 31 mwaka huu, kwenye uwanja wa Uhuru utajumuisha Watanzania wote bila ya kujali dini, kabila wala rangi, kwa lengo la kufanya dua maalum la kuliombea Amani Taifa la Tanzania ikiwa ni mwaka wa 18 tangu kuanza kufanyika mikesha hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkesha huo, Askofu Godfrey Malassy amesema kuwa wametambua shida wanazozipata wakinamama wa Tabora vijijini kwa kujifungua katika giza na hata kusababisha vifo hivyo wanadhamiria kupeleka michango hiyo kununua Solar kwa kusaidia kupunguza adha hizo.

“Zipo njia nyingi za kukusanya michango hii na kuhakikisha inafika sehemu husika ikiwa ni pamoja na kwa njia ya simu, sadaka zitakazokusanywa uwanjani na watu kununua vitabu vya “IJUE SIRI YA AMANI KWA TAIFA” vitakavyomwezesha mtanzania kutambua jinsi gani nchi yetu inaweza kuishi kwa amani” amesema Askofu Mallassy.


Mallasy amesema kuwa Mgeni rasmi wa usiku wa mkesha huo anatarajiwa kuwa rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

No comments: