POLISI
mkoani Rukwa inamshikilia Ofisa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Michael Mwingira ili kusaidia uchunguzi wa magogo 665 na mbao za
mti wa mkurungu vilivyokuwa vinasafirishwa kinyume cha sheria kwenda
China.
Mwingira
ni Ofisa Forodha wa TRA katika Kituo cha Forodha kilichopo kijijini
Kasesya wilayani Kalambo mkoani Rukwa katika mpaka wa Tanzania na nchi
jirani ya Zambia. Hata hivyo, kwa mujibu wa maofisa wa TRA na Misitu
mkoani Rukwa thamani ya magogo na mbao zilizokamatwa haijaweza
kufahamika mara moja.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Magalula Said Magalula alimwamuru Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda kumtia mbaroni ofisa huyo wa TRA ili
asaidie uchunguzi; pia aliamuru ahamishwe mara moja na kupangiwa kituo
kingine cha kazi.
Aidha, amempa wiki moja Ofisa Upelelezi Mkoa wa Rukwa (RCO) awe amekamilisha uchunguzi wa tukio hilo na kumkabidhi matokeo yake.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika Kituo cha Polisi mjini Matai wilayani
Kalambo ambako lori lenye namba ya usajili T 427 ASG aina ya Scania
limekamatwa likiwa limebeba kontena lenye idadi ya magogo 350, Magalula
alisema imebainika magogo hayo yamesafishwa kwa kutumia hati bandia za
mauzo ya nje.
“Tumeshabaini
kuwepo kwa muda mrefu kwa mtandao wa kihalifu unaovuna rasilimali zetu
za misitu, kuandaa nyaraka bandia za kusafirisha magogo nje ya nchi
….usafirishaji wa magogo haya kati ya Tanzania na Zambia ulishapigwa
marufuku kuwa hayaruhusiwi kuuzwa nje ya nchi,” alisisitiza Magalula.
Baada
ya kukagua lori hilo linaloshikiliwa katika Kituo cha Polisi mjini
Matai likiwa na kontena lenye magogo hayo, Magalula aliamuru msafara
wake ufike katika Kituo cha Forodha kilichopo mpakani mwa nchi ya Zambia
katika kijiji cha Kasesya umbali wa kilometa 47 kutoka Matai Mjini.
Katika
Kituo hicho cha Forodha cha Kasesya, Magalula alishangazwa baada ya
kubaini magogo mengine na mbao vyote kwa pamoja vikiwa 315, vikiwa
vimehifadhiwa karibu na jengo la forodha hiyo.
Magogo
hayo yanayodaiwa kuwepo hapo kwa muda mrefu ambapo tayari yalikuwa
yamebanguliwa kwa kusafirishwa China pamoja na mbao zake licha ya
maofisa wa TRA kusisitiza kuwa ni sehemu ya magogo yaliyokamatwa juzi na
kuzuiwa katika Kituo cha Polisi mjini Matai.
“Inasikitisha
sana maofisa wa Polisi , Uhamiaji na mazao ya misitu mlioaminiwa
kuulinda mpaka huu mmeshindwa kufanya hiyo ….. nitawataarifu waajiri
wenu ili wawachukulie hatua za kinidhamu pia kisheria …. Mmeshindwa
kutimiza majukumu yenu ipasavyo,” alisisitiza Magalula.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Wilman Ndile alieleza kuwa miti
ya aina hiyo ya mkurungu ambayo inapatikana kwa wingi wilayani humo
kuliko sehemu nyingine nchini, imepata soko lenye ushindani mkubwa
katika nchi za Mashariki ya Mbali.
“Kamati
ya Ulinzi na Usalama wilayani Kalambo iliweka mtego na kubaini kuwa
miti inaibwa kwa kuvunwa usiku wilayani kwetu kisha inavushwa hadi nchi
jirani ya Zambia na kusafirishwa Mashariki ya Mbali kupitia kituo chetu
cha forodha kiujanja ujanja kwa hati bandia,” alisisitiza DC.
TRA
imekumbwa na kashfa kubwa katika siku za karibuni ukiwamo upotevu wa
makontena zaidi ya 2,800 ambayo hayajalipiwa ushuru wa mabilioni ya
Shilingi, hali iliyosababisha kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani
kwa maofisa wake wa ngazi za juu akiwamo Kamishna Mkuu Rished Bade
aliyesimamishwa kazi na Rais John Magufuli.
No comments:
Post a Comment