WATOA
huduma katika kipindi cha mpito cha mradi wa mabasi yaendayo haraka
jijini Dar es Salaam, kampuni ya UDA-RT wameihakikishia serikali na
wananchi kuwa matayarisho yanaendelea vizuri tayari kwa huduma hiyo
kuanza Januari 10 mwakani.
Ahadi
hii ilitolewa wakati wa ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne
Sagini, alipokuwa akikagua miundombinu katika mabasi yanayotarajiwa
kutoa huduma hiyo.
Siku
chache zilizopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka wahusika wote
wa mradi huo kuhakikisha unaanza mara moja ili kupunguza adha ya
usafiri Dar es Salaam.
“Tulitaka kujiridhisha kama mabasi haya yako tayari kutoa huduma hii,” alisema Sagini mbele ya waandishi wa habari na kuwataka wahusika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa haraka.
Mabasi
140 yanayomilikiwa na kampuni ya UDA-RT yatatumia mfumo wa kisasa wa
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa ukusanyaji nauli, mifumo
ya utoaji taarifa na maeneo maalum ya wazee na walemavu.
Mwenyekiti wa UDA-RT, Robert Kisena aliwataka wananchi kujali mabasi hayo mara huduma itakapoanza.
“Wananchi wajali mabasi haya, madereva nao wana wajibu wa kuhakikisha magari haya yanadumu,” alisisitiza.
Alisema
kuhujumu mabasi hayo mapya au miundombinu ya mradi huo ni sawa na
wananchi kujihujumu wenyewe, kwani huduma hiyo ni kwa ajili yao.
Alisema
tayari kazi ya kufunga vifaa vinavyotakiwa katika mabasi hayo
imeshakamilika kwa baadhi ya mabasi na inaendelea kwa mengine.
Msemaji
wa UDA-RT, Said Mabruk alisema magari yote yanayotakiwa kuanza kwa
huduma hiyo ya mpito yana madereva na walishapewa mafunzo na kwamba ni
matumaini yao kuwa huduma itaanza kwa wakati uliopangwa.
Awamu
ya kwanza inahusisha kilometa 20.9 za njia maalumu kutoka Kimara hadi
Kivukoni, barabara ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo- Gerezani na
sehemu ya barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi njia panda eneo la
Morocco.
No comments:
Post a Comment