NAIBU KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI ALIASA JESHI LA MAGEREZA KUPUNGUZA MATUMIZI YA FEDHA ZA SERIKALI YASIYO MUHIMU - LEKULE

Breaking

16 Dec 2015

NAIBU KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI ALIASA JESHI LA MAGEREZA KUPUNGUZA MATUMIZI YA FEDHA ZA SERIKALI YASIYO MUHIMU

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Mhe. John Mngodo akihubia Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza lililofanyika leo Desemba 15, 2015 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali hapa nchini wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi kama wanavyoonekana katika picha.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua rasmi Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza lililofanyika leo Desemba 15, 2015 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.
Maafisa Wandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka Mikoa yote Tanzania Bara, Makao Makuu ya Jeshi hilo, Wakuu wa Vyuo vya Magereza wakifuatilia majadiliano katika Baraza hilo.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza wakiwa wameshikana mikono huku wakiimba wimbo Maalum wa Mshikamano Daima “SOLIDARITY FOREVER”.
Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Mhe. John Mngodo akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza(walisimama). Wa Pili kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(wa kwanza kushoto) ni Kamishna wa Huduma za Urekebishaji, Deonice Chamulesile(wa kwanza kulia) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa pili kulia) ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi raia wa Jeshi la Magereza, Haikamen Mshida(Picha zote na Lucas mboje wa Jeshi la Magereza).

Na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza

JESHI la Magereza limeaswa kuwa na matumizi mazuri ya fedha za umma ambayo ni pamoja na kuokoa fedha ambazo zilitengwa kwa matumizi ambayo siyo ya muhimu sana na fedha hizo kupelekwa katika mambo muhimu zaidi.

Akizungumza katika ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la Jeshi hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. John Mngodo alisema kwa kufanya hivyo Jeshi hilo litakuwa limeunga mkono kauli ya Rais John Magufuli ambapo Rais amekuwa akisisitiza watumishi wa umma kuokoa fedha za Serikali katika mambo ambayo hayana ulazima.

"Tuzingatie makusanyo ya fedha za Serikali sambamba na kuokoa fedha katika mambo yasiyokuwa ya lazima na kupeleka fedha hizo katika mambo ya muhimu zaidi" Alisema Mngodo.

Mngodo amewataka pia watumishi hao wa Jeshi la Magereza kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na utunzaji wa mali za Serikali.

Aidha aliwasisitiza watumishi hao kuzingatia mapambano dhidi ya Rushwa mahala pa kazi  kwa kuepuka matendo ya utoaji na upokeaji rushwa kwa kuzingatia kauli ya Rais Magufuli kuwa “Tanzania bila ufisadi inawezekana”  badala yake kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza tija mahala pa kazi.

Mngodo katika hotuba yake hiyo aliwataka pia watumishi wa Jeshi hilo waliokuwa kwenye Baraza hilo kuzingatia maadili ya utumishi wa umma wanapodai maslahi yao.

"Natumia fursa hii kuwataka kila mmoja wenu aliyopo hapa kubeba jukumu la kuhakikisha kuwa maadili ya nidhamu katika utendaji kazi kuwa kama chachu ya kuongeza ufanisi inazingatiwa kila siku," alisema Mngodo.

Mngodo alisema katika kuleta maendeleo ni muhimu kuwashirikisha wafanyakazi kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabaraza ya wafanyakazi ili kuweka mikakati ya kuimarisha utendaji kazi na kutatua kero zinazowakabili.

Awali  akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Minja alisema majadiliano ya Kikao hicho yataleta chachu na kuimarisha hali ya watumishi na utendaji kazi  katika Jeshi hilo.
‘’Naamini uwepo wenu hapa utakuwa ni chachu katika majadiliano ambao utasaidia kuimarisha hali za watumishi na utendaji kazi katika Jeshi letu la Magereza” alisema Minja.


Katika Kikao hicho kama ilivyo katika mabaraza ya wafanyakazi, hupokea taarifa za utekelezaji wa Bajeti katika kipindi cha Mwaka 2015/2016 kunaanzia Julai hadi Septemba Mwaka huu ambapo watajadili na kutoa mapendekezo.

No comments: