MBUNGE
wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amekamatwa na polisi eneo la viwanda
(EPZA) Mabibo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Tukio
hilo limetokea kukiwa na mgomo wa wafanyakazi zaidi ya 1800 wa kiwanda
cha nguo cha TZ TOOKU ambao walimpigia mbunge wao aende kutatua mgogoro
huo.
Kubenea alifika katika eneo hilo saa 6 mchana, akakutana na wafanyakazi kusikiliza kero zao za muda mrefu.
Kisha aliamua kuondoka na viongozi wa wafanyakazi hao na kufanya kikao na menejimenti ya kiwanda hicho kuanzia saa 7 hadi saa 9.
Ilipofika
saa 10:30 Makonda alikuja na kupata taarifa kwa muafaka uliofikiwa kati
ya Kubenea, menejimenti na viongozi wa wafanyakazi.
Alitoa
amri wafanyakazi wakusanyike, akaawaambia kesho atafika huko na Waziri
wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Kazi na Ajira, na Waziri wa Afya
Wanawake, Jinsia na Watoto.
Baada
ya kutoa maagizo hayo, Makonda alimzuia Mbunge asihutubie kuaga
wananchi aliokuwa nao tangu mchana, kutokana na hali hiyo Kubenea
alisema ni vema aseme neno, ndipo mvutano ulipoanza.
Makonda
alimuru mkutano ufungwe lakini wafanyakazi hawakutawanyika eneo hilo,
alipoona hivyo aliamrisha Polisi wamkamate Kubenea, kwa madai alimwita
yeye Kibaka.
Katika
tukio hilo, Mwandishi wa habari wa Star Tv aliyekuwa anarekodi tukio
hilo alinyang’anywa kamera na Polisi aliyejulikana kwa jina moja tu la
Denis.
Mwandishi
wa habari Mwanahalisi alijaribu kumsaidia mwenzake ili arejeshewe
kamera lakini Polisi wa kituo cha Magomeni walimtisha, na kumtaka
kuondoka haraka huku wakiondoka na aliyenyang’anywa kamera.
Bado Kubenea anaendelea kuhojiwa na polisi katika kituo cha Magomeni akiwa na mwanasheria wake, Fred Kihwelo.
No comments:
Post a Comment