Wapiga Kura Kibamba Wamtaka Mnyika Kuanza Kufanyia Kazi Ahadi Zake Badala Ya Kuendelea Kutoa Matamko Kwenye Vyombo Vya Habari - LEKULE

Breaking

14 Dec 2015

Wapiga Kura Kibamba Wamtaka Mnyika Kuanza Kufanyia Kazi Ahadi Zake Badala Ya Kuendelea Kutoa Matamko Kwenye Vyombo Vya Habari


Wakazi wa jimbo la kibamba wamemtaka mbunge wao, John Mnyika kuanza kufanyia kazi ahadi zake badala ya kuanza kutoa matamko kwenye vyombo vya habari kuzungumzia mambo ya kitaifa wakati ana mambo kadhaa ya kuyafanyia kazi jimboni kwake.

Wakiongea na mwandishi wa Dar24, wakazi hao wamesema pamoja na kushukuru sana kwa kupewa jimbo jipya ambalo limegawanywa kutoka lililokuwa jimbo la Ubungo, wanatarajia mbunge wao huyo, ambaye kwa kipindi kilichopita pia alitumika katika eneo hilo atakuwa na eneo dogo la kulifanyia kazi hivyo kuwaletea maendeleo kwa kutatua kero zao.

Mkazi kibamba aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Uledi maarufu kama ‘Mzee wa Ukawa’ alisema “Mnyika si mgeni na matatizo ya Kibamba kwani hili lilikuwa ni eneo lake alipokuwa mbunge wa Ubungo. Hivyo hatutegemei kumwona akitumia muda mrefu kuongelea mambo ya kitaifa badala ya kushughulikia kero zetu.”

“Tunamtaka Mbunge wetu arudi jimboni kukaa na sisi ili atueleze mikakati aliyonayo na pia muda wa kuanza kutimiza ahadi alizotuahidi badala ya kuanza kulalamikia suala la ofisi aliyopewa kuwa ndogo. Hivi sasa kipaumbele chake kiwe kero zetu badala ya kufikiria kuanza kukaa ofisini,” alisema Mwanaisha Swedi akiwa katika sehemu yake anayofanyia biashara ya kuuza vitafunio.

"Tunamtaka mbunge wetu aache kulalamikia suala la ofisi, aje atuambie nasi tuna uwezo wa kumjengea ofisi kubwa katika eneo hili. Tunamtaka aje aungane nasi kujikwamua kwenye matatizo yetu ya kiuchumi na kimiundo mbinu" alisema Jerome Munishi ambaye alijitambulisha kuwa ni mkazi wa mbezi mwisho.

Kwa ujumla wakazi wa kibamba wanamtegemea mbunge wao kuacha kuwa mbunge wa matukio na vyombo vya habari kwa kutoa matamko kila jambo la kitaifa linapotokea. 
 
Maelezo ya wakazi hao wa Kibamba yamejikita katika kile wanachoamini kuwa muda wa siasa umepita hivi sasa ni bora akaelekeza nguvu zake katika kufanya kazi kwa kushirikiana na wapiga kura wake.

Credit: Dar24 

No comments: