Kuimarisha
Zao la Karafuu ni sawa na kuimarisha Uchumi na Maendeleo ya nchi,
jitihada za Wadau ni muihimu ili kufika lengo la Serikali la kuifanya
Sekta ya Zao la Karafuu kuwa uti wa mgongo wa Uchumi liweze kufikiwa.
Kutokana
na umuhimu wa Sekta ya Karafuu kwa Maendeleo ya Uchumi Serikali
imefanya mageuzi makubwa katika sekta hiyo kwa lengo la kuongeza
uzalishaji na tija kwa Wakulima na Taifa kwa jumla.
Katika
utekelezaji wa Mageuzi hayo yaliyoanza mwaka 2011 Shirika la Biashara
la Taifa Zanzibar ZSTC ambalo ni mdau mkubwa katika uimarishaji wa Sekta
ya Karafuu ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu (Zanzibar Clove
Fund) ambapo ulizinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein tarehe 28/08/2011.
Baadhi
ya wafanyakazi wa ZSTC wakipita mbele ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali
Mohmaed Shein wakiwa wamebeba bango lenye ujumbe wa kuimarisha zao la
karafuu.
Mfuko
huo wa Maendeleo ya Karafuu umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria mpya ya
Maendeleo ya Karafuu Nam. 2 ya Mwaka 2014, chini ya kifungu Nam. 4 (1)
ambacho kinaipa mamlaka Bodi ya Shirika la ZSTC kuanzisha Mfuko wa
Maendeleo ya Karafuu. Mfuko huo upo chini ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa
Shirika la ZSTC.
Lengo
kuu la kuanzishwa kwake ni Kuimarisha, Kuendeleza na Kusimamia Sekta ya
Zao la Karafuu Zanzibar kwa kutoa msaada unaohitajika kwa Wakulima wa
karafuu kwa lengo la kuongeza uzalishaji.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC Mwanahija Almas Ali
Sekta hiyo ya Karafuu inaendelea kuimarika zaidi hasa baada ya
kuanzishwa kwa Mfuko huo wa Maendeleo ya Karafuu.
Ama
kweli ‘Jembe halimtupi Mkulima’ ni zamu ya Wakulima wa zao la karafuu
kunufaika zaidi na ukulima wa zao hilo kutokana na kuwepo kwa Mfuko huo
wa Maendeleo ya Karafuu unaotoa huduma kwao katika kuimarisha zao la
karafuu.
Bi.
Mwanahija amesema utafiti ulifanyika juu ya namna ya kufanya mageuzi
yenye tija katika Sekta ya Karafuu ndipo ikaoneka umuhimu wa kuanzisha
Mfuko huo ambapo muda mfupi baada ya kuanzishwa unaonekana kuleta faida
katika uimarishaji wa zao hilo. Mfuko huo umeongeza nguvu katika
jitihada za Serikali za kuimarisha zao hilo la uchumi wa Taifa.
“Madhumuni
ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ni kuhakikisha Sekta ya
Karafuu inakua na kuimarika zaidi. Kuongeza idadi ya mikarafuu na
uzalishaji ambapo hivi sasa Wananchi wamehamasika zaidi katika upandaji
mikarafuu kwa wingi”. Amefahamisha Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Bi.
Mwanahija.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC, Mfuko huo
utafanya sensa ya mikarafuu sambamba na kuwasajili Wakulima na
Wafanyabiashara wa zao hilo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Amefahamisha
kuwa kupitia Mfuko huo na kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na
Maliasili kutafanyika tafiti kwenye kila eneo linayohusu zao la karafuu
kwa lengo la kugundua changamoto na kuzifanyia kazi.
Amesema
Shirika la ZSTC kwa kushirikiana na Wadau wengine inakamilisha mpango
maalumu wa kuziongezea hadhi na thamani karafuu za Zanzibar kupitia
mradi wa ‘Branding’ ili kuongezeka kwa uzalishaji kwenda sambamba na
kuongezeka kwa tija kwa Wakulima na Taifa.
Amesema
hivi sasa mpango huo upo katika kutafuta vinasaba vinavyoonyesha ubora
wa karafuu za Zanzibar kupitia Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar.
Wakati
akizindua Mfuko huo Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohmed Shein alihimiza
suala la utafiti katika kila sehemu inayohusu kilimo na biashara ya Zao
la Karafuu na kusisitiza suala la kuongeza thamani ya za karafuu
sambamba na kuzingatia viwango ili kulinda ubora wa Zao hilo.
Aidha,
Mkurugenzi amefahamisha kuwa Mfuko huo umekuwa ni msaada mkubwa katika
uimarishaji wa zao la karafuu hasa kwa Wakulima ambapo unatoa fidia kwa
Wakulima wanaopata ajali wakati wa uchumaji kupitia Shirika la Bima
Zanzibar.
Mfuko
huo ni neema kwa Wakulima wa karafuu kwa namna unavyowanufaisha na
kubadilisha maisha yao ya kila siku katika zao la karafuu. Mfuko huo
inaonekana umedhamiria kuwapatia Wakulima vifaa na huduma zinazohitajika
katika uzalishaji.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC, vikundi vya uatikaji miche ya
mikarafuu vya binafsi na Serikali huwezeshwa kwa kupatiwa vifaa vya
uatikaji miche kama vile vifuko (Polythen bage), mabero, mipira ya maji
na matenki.
Hurahisishiwa
upatikanaji wa vifaa vya uanikaji na uchukuaji wa karafuu kama vile
majamvi na magunia na kupatiwa ruzuku kulingana na utaratibu maalum
uliowekwa.
Amesema
Mfuko huo umelipa bima ya milioni 60 kwa Shirika la Bima ili kuwafidia
Wakulima 100 wanaokisiwa kupata ajali katika zoezi la uchumaji wa
karafuu mwaka 2015/2016 ambapo hadi sasa tayari watu tisa wameripotiwa
kupata ajali wote kutoka Pemba.
Amesema
Wakulima wanaendelea kupata mikopo ya uchumaji kupitia Mfuko huo na
alifahamisha kuwa katika bajeti ya 2015/2016 Mfuko umepanga kutumia
milio 140 kwa ujenzi wa barabara ya Ng’omeni ikiwa ni msaada wa kusadia
miundombinu ya sehemu za uzalishaji wa karafuu.
Amesema
kupitia Mfuko huo Shirika limeongeza jitihada za kutoa elimu kwa
Wakulima juu ya uchumaji na uanikaji unaotakiwa ili kulinda ubora wa zao
hilo katika soko la nje.
Mfuko
huo ni moja ya nyenzo muhimu za kuimairisha na kuendelza zao la karafuu
ambapo Wananchi hasa Wakulima wa zao hilo wana kila sababu ya kujivunia
mafanikio yaliyopatikana katika kulirejeshea hadhi hilo la biashara.
Pamoja
na juhudi hizo bado Sekta ya Karafuu inakabiliwa na changamoto nyingi
zinazohitaji kufanyiwa kazi. Moja ya changamoto hizo ni kwa baadhi ya
Wakulima kuchafua karafuu kwa makusudi, kuendelea kuanika karafuu
barabarani, juu ya bati na sakafuni licha ya kupewa elimu juu ya madhara
ya kuanika katika sehemu hizo.
Makosa
hayo ni hatari kwa vile yanaweza kusababisha Wanunuzi katika soko
kuzikataa na hivyo kupelekea hasara kwa Wakulima, Wananchi na Taifa kwa
jumla.
Ni
jukumu la jamii kusaidia katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulinda
ubora wa karafuu zetu za Zanzibar ili kufanikisha azma ya Serikali ya
kuifanya Sekta ya Karafuu kuwa ni Sekta ya kukuza uchumi wa Nchi na
yenye kujenga ustawi wa wananchi wake.
“Kithamini
kikutunze” ni msemo maarufu wanaoutumia wahenga wa Kiswahili juu ya
utunzaji na kuthamini mambo muhimu yanayoleta tija kwa jamii. Kuna kila
haja kwa Wakulima wa karafuu kuzithamini na kuzitunza karafuu kwa
manufaa yao na Taifa kwa jumala.
.
Changamoto
nyengine ni katika uzalishaji ambapo mahitaji ya miche ni makubwa zaidi
kuliko uwezo wa kuotesha, huduma dhaifu kwa mikarafuu michanga na
baadhi ya Wakulima kutaka miche mingi kuliko uwezo wa kuipanda na
kuihudumia.
Mabadiliko
ya tabia nchi nayo yamekuwa ni changamoto kubwa ambapo yanayosababisha
miti mingi kukauka ikiwemo mikarafuu na ongezeko la mahitaji ya ardhi,
majengo na kuni na upandaji usiozingatia taaluma.
Mfuko
wa maendeleo ya Karafuu ni chachu ya kuongeza uzalishaji wa zao la
karafuu Zanzibar ili kurudi katika kiwango cha zamani ambapo historia
inaonyesha kuwa Zanzibar ilikuwa nafasi ya kwanza duniani katika
uzalishaji wa karafuu nyingi ila kwa sasa ipo nafasi ya tatu.
“Karafuu ni Uhai’ Karafuu kwa Maendeleo ya Zanzibar”
No comments:
Post a Comment