Mahakama Yatupa Pingamizi la Ubunge dhidi ya Dk Mwakyembe - LEKULE

Breaking

29 Dec 2015

Mahakama Yatupa Pingamizi la Ubunge dhidi ya Dk Mwakyembe


Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, imetupilia mbali shauri la kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi wa ubunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe(CCM).

Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa jimbo hilo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chadema, Abraham Mwanyamaki baada ya kushindwa kulipa Sh3 milioni ambazo ni dhamana ya kesi kwa anaowalalamikia.

Sheria ya kesi za kupinga matokeo ya ubunge inamtaka mlalamikaji kulipa dhamana ya Sh5 milioni kwa kila anayemlalamikia, ambapo Mwanyamaki alitakiwa kulipa jumla ya Sh15 milioni kwakuwa aliokuwa akiwalalamikia walikuwa watatu.

Hata hivyo Mwanyamaki baada ya kuomba huruma ya mahakama alipunguziwa hadi Sh1 milioni kwa kila mlalamikiwa. Jumla alitakiwa alipe Sh3 milioni.

Pia Mahakama hiyo imeamuru Mwanyamaki kulipa fidia ya gharama za walizotumia walalamikiwa katika kesi hiyo, ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kyela, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Dk Mwakyembe.

Mwanyamaki ni miongoni mwa waliokuwa wagombea wa mkoani Mbeya, ambao walifungua kesi mahakamini hapo, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita.

Wengine ni Liberatus Mwang’ombe (Chadema) dhidi ya mbunge Haroon Pilmohamde wa CCM (Mbarali), John Mwambigija (Chadema), dhidi ya Saul Amoni wa CCM (Rungwe), Dk Luca Siame (CCM) dhidi ya David Silinde wa Chadema (Momba), Adam Zella (Chadema) dhidi ya Oran Njeza wa CCM (Mbeya Vijijini) na Fanuel Mkisi (Chadema) dhidi ya Jophet Hasunga wa CCM (Vwawa).

Jaji wa mahakama hiyo, Atuganile Ngwala alitoa uamuzi huo jana mahakamani hapo baada ya wakili wa Mwanyamaki, Benjamini Mwakagamba akisaidiana na Adrian Mhina kudai mahakamani hapo kwamba mteja wao alishindwa kutoa kiasi hicho alichotakiwa kulipa ili kesi ya msingi iweze kuendelea, hivyo wanaiachia mahakama iweze kutoa uamuzi wake juu ya suala hilo.

Baada ya maelezo Jaji Ngwala akatoa nafasi kwa wakili aliyekuwa akimtetea Dk Mwakyembe, Mpale Mpoki aliiomba mahakama imuamuru Mwanyamaki awalipe gharama walizotumia tangu kesi ndogo ianze kulizikilizwa mahakamani hapo.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Ngwala alisema ameridhika na hoja ya wakili Mpoki, na kusema licha ya Mwanyamaki kushindwa kulipa gharama hiyo na kesi kufutwa haina maana kwamba hatatakiwa kulipa gharama nyingine.

“Mahakama inamtaka mdai (Mwanyamaki) kulipa gharama zote kwa washtakiwa wote watatu aliowashtaki kwani ndiye aliyeleta pingamizi hilo. Na kushindwa kwake kulipa kiasi cha Sh3 milioni tatu na kesi kuondolewa mahakamani hapa haimaanishi hatatakiwa kulipa fidia hizo,” alisema Jaji Ngwala.

Katika hatua nyingine, Jaji Ngwala alisema walalamikaji wengine walikamilisha taratibu zote walizotakiwa ikiwamo kulipa Sh3 milioni, ili kesi ya msingi ianze kusikilizwa kama ambavyo walioomba kwenye kesi ndogo ya kuomba kupunguziwa gharama kutoka Sh5 milioni kwa kila mshtakiwa hadi Sh1 milioni kwa kila mmoja.


Alisema Januari 7 kesi hizo zitapangiwa majaji kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, ambapo walalamikaji, Liberatus Mwang’ombe wa Jimbo la Mbarali, John Mwambigija wa Rungwe, wanatetewa na mawakili Benjamini Mwakagamba na Adrian Mhina, Fanuel Mkisi wa jimbo la Vwawa anatetewa na mawakili Magreth Lyatuu na Boniface Mwabukusi.     

No comments: