MAAFISA MAGEREZA NCHINI WAMETAKIWA KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA - LEKULE

Breaking

17 Dec 2015

MAAFISA MAGEREZA NCHINI WAMETAKIWA KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA


 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Mhe. Mbarak Abdulwakil akihutubia kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza uliofanyika leo Desemba 16, 2015 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Maafisa Magereza,Ukonga jijini Dar es Salaam.
 Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali hapa nchini wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi kama wanavyoonekana.
 Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza uliofanyika leo Desemba 16, 2015 katika Ukumbi wa Bwalo Kuu la Maafisa Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam.
 Meza Kuu wakiwa kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza.




 Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(wa kwanza kulia) akiteta pamoja na Makamishna wa Jeshi la Magereza kabla ya kumpokea mgeni rasmi(wa kwanza kulia) ni Naibu Kamishna wa Magereza Mstaafu, John Nyoka.

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Mhe. Mbarak Abdulwakil akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza (walisimama). Wa Pili tatu kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja(wa tatu kulia) ni Kamishna wa Huduma za Urekebishaji, Deonice Chamulesile(wa pili kulia) ni Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga(wa pili kushoto) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(Picha zote na Lucas mboje wa Jeshi la Magereza).


Na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza.
MAAFISA wa Magereza nchini wametakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kulingana na kauli mbiu ya Rais wa awamu ya tano, Dkt. John Magufuli.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak Abdulwakil amesema kila kiongozi afanye kazi kwa bidii na maarifa ili utendaji wake ulete tija mahala pa kazi.

"Nadhani kila mmoja anafahamu kauli mbiu ya Mhe. Rais wa awamu ya tano ya "hapa kazi tu", na amekuwa akisisitiza kuwataka viongozi wenye dhamana na kila Mtanzania kufanya kazi kwa bidii na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani huu ni wakati wa kazi tu, " alisema.

Vile vile, Bw. Abdulwakil amewataka katika mkutano huo kujadili kwa kina mada maalum itakayowasilishwa na Kamishana Jenerali wa Magereza na kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji katika sekta za Kilimo, Mifugo na Viwanda.

"Kwa vile Jeshi la Magereza ni mdau mkubwa wa uzalishaji hasa katika sekta za Kilimo, Mifugo na Viwanda vidogo vidogo, nawaasa katika mkutano huu mjadili kwa kina na mapana hatimaye mtoke na mkakati wa namna mtakavyoongeza uzalishaji katika sekta hizo " alisema. 

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja amesema Jeshi la Magereza limejipanga vyema kutekeleza maelekezo mbalimbali ambayo yalitolewa na Rais wa Awamu ya tano, Mhe. John Magufuli ambayo ni pamoja na kuanzisha miradi ya kibiashara ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuwahudumia wafungwa na mahabusu magerezani.

"Kuna mashamba 11 yametengwa ili kuzalisha kibiashara hivyo kuipunguzia Serikali mzigo na pia tumeainisha na miradi ya ufugaji" alisema Minja.

Kamishna Jenerali Minja amesema kuwa Jeshi hilo linakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo madeni ya Wazabuni, ukosefu wa Ofisi za Wakuu wa Magereza Mikoa, Migogoro ya Ardhi na wananchi wanaoishi jirani na vituo vya magereza pamoja na Msongamano wa wafungwa magerezani. 

Mkutano huu ni wa kwanza kufanyika tangu Uongozi wa Serikali ya awamu ya tano uingie Madarakani chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli mapema mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2015.

Akizungumza kuhusu mkutano huo alisema ni mkutano wa kila mwaka kwa ajili ya kutathimini kwa pamoja utendaji wa Jeshi katika maeneo yote na kuweka mikakati ya kukabiliana na matatizo yaliyopo, kurekebisha dosari zilizojitokeza na kujiwekea malengo ya kuboresha utendaji wa kazi kwa ujumla katika mwaka ujao. 

No comments: