Kasi
ya Mawaziri wa Rais John Pombe Magufuli kufanya ziara za kushtukiza na
kutoa maagizo kwa watendaji imeanza kufumua uozo baada ya jana
kubainika kuwa watumishi 219 kati ya 704 wa serikali wameajiriwa kwa
vyeti vya kughushi.
Sakata hilo liliibuliwa baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki kutembelea Idara,vitengo vya Usimamizi wa Rasilimaliwatu (Utumishi) na kuagiza hatua kali zichukuliwe kwa wote waliobanika kutumia vyeti visivyo vyao kupata ajira serikalini.
“Watumishi
wote waliobainika kupitia Mfumo Shirikishi wa Malipo ya Mishahara ya
Watumishi wa Umma (Payroll), kwamba wametumia vyeti visivyo halali
wachukuliwe hatua stahiki,” amesema Kairuki.
Amemtaka
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa RasilimaliwatuUtumishi, Emmanuel
Mlay kutafuta ufumbuzi wa kumaliza tatizo la watumishi wanaotumia vyeti
vya kughushi.
“Muwasilishe
vyeti vyao Baraza la Mitihani kwa ajili ya uhakiki na baada ya uhakiki
muwachukulie hatua stahiki watumishi wanaoonekana kutumia vyeti visivyo
halali kwao,” alisisitiza.
Naye,
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa RasilimaliwatuUtumishi,
Leonard Mchau, alisema kuwa Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, imehakiki watumishi 704 na kati ya hao, watumishi 219 baada ya
vyeti vyao kuhakikiwa na Baraza la Mitihani, waligundulika waliajiriwa
kwa vyeti vya kughushi.
Hata
hivyo, Mchau aliongeza kuwa baadhi ya watumishi hao waliobainika
kughushi vyeti ili kujipatia ajira serikalini, wamekimbia vituo vyao vya
kazi. Mchau aliwaasa wananchi kuepuka mchezo wa kughushi vyeti, ili
kujipatia ajira Serikalini.
“Ni
kosa la jinai kughushi vyeti kwa lengo la kujipatia kazi, sasa endapo
utagundulika umeghushi vyeti, utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za
nchi,” alifafanua Mchau.
Kwa
sasa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma inaendelea na
uhakiki wa vyeti kwa watumishi wote wa umma nchini mpaka kila mmoja
atakapohakikiwa.
No comments:
Post a Comment