Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga atafanya ziara ya kikazi ya siku
mbili mkoani Arusha kuanzia leo Jumamosi tarehe 19 Desemba 2015.
Atakapokuwa
mkoani Arusha, Balozi Mahiga atafanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. Richard Sezibera. Mazungumzo yao
yatahusu namna ya kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.
Aidha,
Mhe. Waziri atatembelea eneo la Lakilaki ambalo limetengwa na Serikali
kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za taasisi za kimataifa. Ujenzi unaoendelea
hivi sasa kwenye eneo hilo ni jengo la ofisi la taasisi ya Mechanism
for Crime Tribunals (MICT) inayorithi shughuli za Mahakama ya Kimataifa
ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ambayo itakamilisha shughuli zake
tarehe 31 Desemba 2015.
Mhe.
Waziri pia atatembelea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha
(AICC) kuonana na uongozi wa Kituo hicho kwa madhumuni ya kufahamiana.
AICC ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Mhe. Waziri atarejea jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili tarehe 20 Desemba 2015.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
18 Desemba, 2015
No comments:
Post a Comment