Chadema ‘Wapotezea’ Ahadi ya Kuuza gari la Meya - LEKULE

Breaking

9 Dec 2015

Chadema ‘Wapotezea’ Ahadi ya Kuuza gari la Meya


MADIWANI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameipotezea ahadi ya kuuza gari la kisasa lililokuwa likitumiwa na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi (CCM) waliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Wakati wa kampeni hizo, madiwani hao pamoja na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa walisema wataliuza gari hilo la kisasa aina ya Toyota Land Cruiser Prado ili fedha zitakazopatikana zitumike kununua gari la kubeba wagonjwa kwa ajili ya hospitali ya manispaa hiyo.

Hospitali hiyo inayotoa huduma wakati ujenzi wake ukiendelea imejengwa ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.

Katika kampeni hizo, wagombea hao wa Chadema waliwalaumu waliokuwa madiwani wa Halmashauri ya Manispaa hiyo 2010-2015 ambao kwa asilimia 99 walichaguliwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupitisha uamuzi waliouita wa kipuuzi wa kununua gari hilo huku hospitali hiyo ikiwa haina gari la kubeba wagonjwa.

Katika mikutano yao mbalimbali ya kampeni, Chadema waliwaomba wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini wamchague mgombea wao ubunge na wagombea wake ili wakafanye maamuzi mengi yenye maslahi mapana kwa wapiga kura ikiwa ni pamoja na kuuza gari hilo ili fedha zake zikanunue gari la kubeba wagonjwa.

Ahadi hiyo na nyingine nyingi za chama hicho zilipokelewa na wapiga kura wa mjini Iringa kwa kumchagua kwa awamu nyingine ya miaka mitano Mchungaji Msigwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini na kuwachagua madiwani 14 kati ya 18 wa jimbo hilo, kuunda halmashauri ya manispaa hiyo.

Wakizungumza na wanahabari hivi karibuni, Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe na Naibu wake Joseph Lyata walisema mpango wa kuuza gari hilo haupo tena kwa sababu taratibu za kupata gari la wagonjwa zinaendelea kufanywa kwa kasi kubwa.

“Ni kweli kulikuwa na ahadi ya kuuza gari hili ili fedha zake zitumike kununua gari la wagonjwa, mpango huo haupo tena kwa sababu kuna mipango mingine ya kupata fedha zitakazotumika kununua gari rasmi la wagonjwa,” alisema Naibu Meya Lyata.

Lyata alisema kwa kuzingatia mpango huo, gari hilo litaendelea kutumika kwa matumizi ya Meya, Naibu wake na kwa shughuli nyingine za halmashauri pale inapolazimu.


Alisema halmashauri yao itahakikisha inavipitia vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo, zikiwemo kodi mbalimbali, na makusanyo yake yatatumiwa kununua gari la kubeba wagonjwa sambamba na kuongeza gari lingine la kubeba taka ili kuufanya mji wa Iringa uendelee na sifa yake ya usafi.

No comments: