MAKAMU
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala
amesema wanafunzi wawili wa chuo hicho Kampasi ya Mlimani walioripotiwa
kuumwa tumbo, hawana ugonjwa wa kipindupindu, bali walipata adha hiyo
baada ya kula kwenye mgahawa wa Cafeteria One chuoni hapo.
Alitoa
ufafanuzi huo jana Dar es Salaam kutokana na uvumi kwamba ugonjwa wa
kipindupindu umeingia chuoni hapo na tayari baadhi ya wanafunzi wanaugua
ugonjwa huo.
Akizungumzia
hilo, Profesa Mukandala alisema ni kweli wanafunzi wawili miongoni mwa
wanafunzi waliokula chakula katika moja ya Cafeteria chuoni hapo,
walipata shida ya kuumwa tumbo na kupelekwa kwenye hospitali ya chuo kwa
matibabu.
Alisema
baada ya uchunguzi, ilibainika wanafunzi hao hawakuwa na ugonjwa wa
kipindupindu, bali walipata maradhi ya tumbo kutokana chakula hicho.
“Walipimwa
na hawakuwa na tatizo la kipindupindu, ila huyu mzabuni anayehudumia
Kafteria One ana matatizo na usafi, na tulishamsitisha kutoa huduma, ila
alikimbilia mahakamani na kurejeshwa,” alisema Profesa Mukandala.
Alisema
baada ya kurudishwa uongozi umeamua kumuacha, kwani mkataba wake
unaisha mapema mwakani na kusema utakapoisha hawataendelea naye,
akisisitiza kuwa, pamoja na kuwa na matatizo ya usafi, pia alikiuka
maagizo ya kuongeza bei ya vyakula bila taarifa.
Hata
hivyo, Profesa Mukandala amewasisitiza wanafunzi chuoni hapo
kuhakikisha wanazingatia usafi ili kujiepusha na maambukizi ya maradhi
na kuutaka pia uongozi wa mgahawa huo, kuhakikisha wanazingatia usafi na
kuboresha vyakula, kwa kuwa wanahudumia jumuiya kubwa
No comments:
Post a Comment