Ahadi ya JPM ya ujenzi wa reli kuanza - LEKULE

Breaking

29 Dec 2015

Ahadi ya JPM ya ujenzi wa reli kuanza


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameanza ziara mkoani Kigoma huku akiahidi kuanza ujenzi wa reli mpya ya kisasa ya viwango vya ‘standard gauge’, itakayosaidia kuimarisha biashara ya kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kupitia Bandari ya Kigoma.
Tamko la Waziri Mkuu Majaliwa inaashiria kuanza kwa utekelezaji wa vipaumbele 25, ikiwamo ujenzi wa reli ya kati, alivyovitoa Rais John Magufuli (wakati huo akiwa mgombea urais wa CCM), Agosti 24, wakati wa uzinduzi wa kampeni zake kwenye Viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wakazi wa Kigoma katika Mwalo wa Kibirizi, Waziri Mkuu Majaliwa alisema mradi huo utaambatana na ujenzi wa bandari kavu eneo la Katosho mjini Kigoma, kwa ajili ya kushusha mizigo inayosubiri kwenda nje ya nchi.
“Lazima tujenge reli ya kisasa na tumezindua ujenzi wa reli ya urefu wa kilomita mbili. Huwezi kuimarisha bandari kama reli itakuwa imechoka na hii ilijengwa miaka 100 iliyopita, sasa imezeeka haifai, ndiyo maana tumeamua kutumia fedha nyingi kuhakikisha mradi huu wa reli ya kisasa na ujenzi wa bandari unakamilika kwa wakati,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Katika maelezo yake hayo Majaliwa alipokea kilio cha wakazi wa Katosho inakotakiwa kujengwa bandari kavu wanaolalamika kupunjwa malipo ya fidia ya nyumba na mazao, aliwahakikishia kuwa mchakato wa kutathmini unarudiwa hivyo aliwashauri wananchi waliopokea fedha za fidia kuhama ili kupisha ujenzi wa bandari.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wavuvi na wafanyabiashara kutumia fursa ya Mwalo wa Kibirizi, ambalo linapokea mazao ya uvuvi na kuyachakata kwa ajili ya kuingia sokoni, jambo litakalosaidia kuinua uchumi na kuongeza thamani ya mazao hayo.
Alisema Serikali itatafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuuza samaki na dagaa wanaovuliwa kutoka Ziwa Tanganyika na kuwezesha wavuvi kujiongezea kipato, hali itakayowafanya wawe na uwezo wa kununua zana bora za uvuvi na kuongeza kiwango cha uvuvi.
Pia aliahidi kumuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu kuongeza ulinzi Ziwa Tanganyika ili kupambana na maharamia wanaopora zana za uvuvi, ambapo pia amemuagiza mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya kufanya kikao na Balozi wa Congo DRC ili kuona njia bora ya kushirikiana kupambana na maharamia.

No comments: