Dar/Mikoani. Baada ya Rais John Magufuli kuanza kwa kishindo
maisha ya Ikulu kwa kutekeleza kauli mbiu yake ya “hapa kazi tu”, watu
walioongea na gazeti hili wameonyesha kuridhishwa, lakini baadhi
wakimpinga na wengine kumkosoa.
Akiwa kwenye kampeni za
kuutaka urais kwa tiketi ya CCM, alisema ataanza kazi mara baada ya
kuapishwa, na atafanya kazi usiku na mchana.
Katika
siku nne za kwanza, Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano pia ametoa
maagizo kadhaa, ikiwemo kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
kuhakikisha inakusanya kodi hasa kwa kuwabana wafanyabiashara wakubwa,
kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kutangaza elimu bure kuanzia mwakani.
Rais
Magufuli alitoa agizo hilo baada ya kufanya kikao na makatibu wakuu,
naibu makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu na Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade kwa lengo la kutoa
mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Alisema
mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi huko nje, ndiyo watakaotakiwa
kufanya shughuli zote kwenye nchi wanazofanya kazi hadi hapo
atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine.
Wasemavyo wasomi
Wengi
waliozungumza na gazeti hili walimsifu Rais Magufuli kutokana na
kuagiza walipa kodi, hasa wafanyabiashara wakubwa wadhibitiwe,
kusimamisha safari za nje, wakisema fedha zitakazookolewa zitasaidia
katika kutekeleza ahadi ambazo yeye na chama chake walizitoa wakati wa
kampeni.
“Ingawa kitaalamu huwezi kupima utendaji kwa
siku tatu, Rais Magufuli ameanza kazi kwa kutoa maagizo ili kuhakikisha
anatekeleza aliyoahidi kama kutoa elimu bure ya msingi hadi sekondari,”
alisema Profesa Lugano Kusiluka wa Chuo Kikuu Huria (OUT).
“Sasa ni wajibu wa watendaji wa serikali kutekeleza.”
Sifa
kama hizo zilitolewa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Charles
Marwa, ambaye alisema hatua ya kuanzia kuwabana walipa kodi wakubwa ni
mwanzo mzuri, akishauri Dk Magufuli aanze kuwabana maafisa wa juu wa TRA
ndipo ashuke kwa maafisa wa chini kudhibiti kodi.
Suala
la kodi pia lilizungumziwa na Dk Alexander Makulilo wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam ambaye alisema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa ndiyo
wakwepaji wakubwa wa kodi.
“Wakati wafanyakazi wenye
mishahara mikubwa ndiyo wanaolipa kodi kubwa serikalini, baadhi ya
wafanyabiashara wakubwa ndiyo wanaoongoza kukwepa na kusamehewa kodi,”
alisema.
Alitaka juhudi kubwa ifanyike katika kuhakikisha wafanyabiashara hao hawakwepi kodi wala kupewa misamaha.
Kwa
upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho
alisema Dk Magufuli ameanza kazi vizuri kutokana na kuchukua hatua
zinazolenga kuhakikisha Serikali inakuwa na fedha.
Alisema
chama chake cha CCM kilitoa ahadi nyingi kwa wananchi wakati wa kampeni
na hivyo ili kutimiza ahadi hizo ni lazima kodi zikusanywe na kubana
matumizi ya Serikali.
Dk Benson Bana, mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, pia alipongeza uamuzi wa kudhibiti walipa kodi
akisema kama kila mmoja angekuwa analipa, nchi isingekuwa na utegemezi
katika bajeti kama uliopo sasa.
“Wafanyabiashara wengi
hawalipi kodi, wanashirikiana na wafanyakazi wenye dhamana ya kukusanya
kodi kukwepa kodi, wanagawana fedha za Watanzania. Kama Rais Magufuli
ameliona hilo, basi huo ni mwanzo mzuri,” alisema.
Dk
Bana pia alisema Rais anatakiwa kuangalia eneo la matumizi ya magari kwa
watumishi wa Serikali na kushauri walipwe posho ya mafuta badala
kutumia magari ya kifahari ambayo alisema yanatafuna fedha nyingi za
walipa kodi.
“Wanaotakiwa kutumia magari ya Serikali ni
mawaziri na manaibu wao, makatibu wakuu, manaibu wao na wakurugenzi
waandaliwe utaratibu mwingine wa kupewa posho ya usafiri ili watumie
magari binafsi,” alisema.
Alisema hivi sasa inawezekana
bosi akawa anaishi Bunju na dereva wake Mbagala ambako ndiko gari
linakolala, hali ambayo alisema inasababisha kuwa na gharama kubwa za
uendeshaji.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George
Shumbusho alisema iwapo Serikali ya Dk Magufuli itawategemea
wafanyabiashara wadogo walipe kodi, haitaweza kutekeleza ahadi zake kwa
sababu hakutakuwa na fedha.
Edward Porokwa, ambaye ni
mkurugenzi wa shirika la PINGOs Forums, alisema kutaka walipakodi
wakubwa walipe kodi, ni jambo zuri ambalo litaondoa misamaha ya kodi
inayoliangamiza taifa.
Safari za nje hazina tija
Wachambuzi
hao pia waliangalia agizo la kusitisha safari za nje hadi kwa kibali
maalumu na kutaka shughuli ambazo zingefanywa na watendaji waliopo hapa
nchini, zifanywe na mabalozi.
“Mabalozi sasa watakuwa
na majukumu zaidi katika kuwakilisha nchi nje,” alisema Martine Masawe,
mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye alimsifu Rais kwa uamuzi wa
kusitisha safari za nje.
Alisema njia hiyo itapunguza
matumizi makubwa ya nchi na kufanya fedha kuwa na matumizi katika
masuala ya kusaidia vipaumbele vilivyopo.
Maoni hayo
yanalingana na ya Dk Alexander Makulilo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM)aliyesema safari za nje zimekuwa zikitumia fedha nyingi za
walipakodi wakati kuna mabalozi wanaowakilisha nje ya nchi.
“Nashauri
yeye ndiye awe mfano kwa kupunguza safari zake nje kwa sababu Rais na
ujumbe wake hutumia gharama kubwa katika safari za nje,” alisema.
Lakini
Dk Bana alikwenda mbali zaidi kwa kusema Rais anatakiwa kushikilia
msimamo wake kwa kuwa suala la safari za nje limekuwapo tangu Serikali
ya Awamu ya Kwanza.
“Ikulu ndiyo ilikuwa inatoa vibali
kwa watumishi wanaosafiri kwenda nje ya nchi, lakini usimamizi umekuwa
mbaya na kusababisha watumishi kusafiri mara kwa mara nje ya nchi kwenye
mikutano ambayo wakifika wala hawachangii chochote,” alisema Dk Bana
ambaye amebobea kwenye sayansi ya siasa.
“Ameanza kazi
vizuri kwa sababu eneo la safari za nje linapoteza fedha nyingi wakati
watumishi wengi wanakwenda huko kwa ajili ya kufanya manunuzi.”
Pia
Faraja Christotoms, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm),
alimtahadharisha kuwa maagizo hayo yasiwe nguvu ya soda.
“Kasi aliyoanza nayo siyo mbaya, tunaomba tu isiwe kama nguvu ya soda,” alisema.
“Hata
Rais (wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete alianza hivyo hivyo
kwa kutembelea wizara mbalimbali. Lakini hawa ni watu wawili tofauti.
Tumpe muda tuone, labda ana dhamira nzuri na nchi yake.”
Hoja za wanaomkosoa
Maagizo na utendaji wa Rais katika siku zake nne za kwanza hayajakosa wakosoaji.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Losolutie alisema agizo la kutoa
elimu bure linahitaji kwenda sambamba na vifaa vya elimu.
“Hata
kama watasema elimu bure wakati bado shule hazina madawati na walimu
hawalipwi vizuri itakuwa haina maana kusema elimu ni bure wakati
wanafunzi katika fomu zao za kujiunga na shule wataambiwa waje na
mchango wa maabara, madawati, mafyekeo, walinzi na majembe,” alisema.
Alishauri
utekelezaji wake uwe ni pamoja na kufuta michango ya wazazi, akisema
kwa sasa ada ya shule hizo ni Sh 20,000, lakini michango ya mwanafunzi
anayeingia kidato cha kwanza inafikia Sh300,000 jambo ambalo ni mzigo
kwa mzazi kuliko ada.
Mwanafunzi wa Chuo cha Mipango
Dodoma, Godrick Ngoli, alisema uamuzi wa kutoa elimu bure ni mzuri,
lakini ingefaa zaidi baraza la mawaziri kushirikishwa kwanza ili kupanga
mipango ya utekelezaji wake kwa pamoja.
Mwingine
aliyemkosoa ni Profesa Semboja ambaye alisema Dk Magufuli alitakiwa
kwanza kuhakikisha mifumo yote ya Serikali inafanya kazi vizuri kwa
namna inavyotakiwa.
Alisema iwapo Rais atafuatilia kila kitu, itafikia wakati atachoka na kuona mzigo mkubwa.
Alimshauri
atumie siku 100 za kwanza kusoma mifumo inavyofanya kazi na kuwapa
majukumu watendaji wake ili kurekebisha kasoro atakazokuwa amezibaini.
“Urais
ni taasisi, na siyo kwamba Rais atafanya kila kitu mwenyewe. Rais
Magufuli ahakikishe anakuwa na timu nzuri ya watendaji ambayo itamsaidia
kusimamia yale yote anayotaka yafanyike bila yeye kusema neno,”
alisema.
Pia, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Paul
Rosolutie alitilia shaka utekelezaji wa elimu bure na kusema suala hilo
linahitaji muda wa kutosha ili kuweka mipango ya utekelezaji wake bila
kuathiri huduma nyingine muhimu kwa shule za umma.
“Hata
zile Sh20,000 wanazolipa wanafunzi zilikuwa hazitoshi kutatua matatizo
ya shule na Serikali inashindwa kupeleka fedha za wanafunzi. Sidhani
kama hilo lilifanyika, vinginevyo itakuwa ni mzigo mkubwa kwa watendaji
wa Serikali katika kulitekeleza,” alifafanua.
Wapinga kusitishwa safari
Marwa
wa Chuo Kikuu cha Mzumbe pia alipinga uamuzi wa kusitisha safari za nje
akisema utasababisha matatizo kwa kuwa makubaliano mengi ya nchi
huhusisha mawaziri na watumishi wa Serikali.
“Sasa kusema mabalozi ndiyo watakuwa wanawakilisha nchi katika baadhi ya mambo haitawezekana,” alisema.
Marwa
alitoa mfano Rais aliyepita aliyesitisha safari zote za nje isipokuwa
kwa kibali cha Serikali wakati akiingia madarakani mwaka 2005, lakini
akakumbana na ugumu katika utekelezaji wa agizo hilo, na badala yake
safari zikaongezeka.
Maoni ya wananchi
Wananchi wengine walioongea na Mwananchi pia walisifu hatua ambazo Dk Magufuli ameshachukua hadi sasa.
Mwenyekiti
wa Kampuni za Ulinzi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kasimir Kubaja
alisema kuzuia safari za viongozi nje ya nchi ni safi kwa sababu
zinatumia fedha nyingi za kigeni wakati ukweli wapo mabalozi ambao
wangeweza kutekeleza majukumu hayo.
Hata hivyo Kubeja
alimshauri Rais Magufuli kufuatilia kwa ukaribu suala la wazabuni
serikalini akisema fedha nyingi zinaibwa katika manunuzi.
Naye
mhandisi wa umeme wa mjini Mbeya, George Mwang’ombe alisema kitendo cha
kusitisha safari za nje kwa viongozi ni kizuri, lakini kiende sambamba
na kupiga marufuku magari ya Serikali kwenda kwenye baa, kuzuia posho za
vikao vya ndani na kuwabana watendaji wa halmashauri wafanye kazi za
wananchi.
Mwang’ombe pia alishauri Serikali itoe fedha
za uendeshaji kwenye shule za sekondari na za msingi ili kuepusha ukata
utakaosababishwa na kutolewa elimu bure.
Mkurungezi wa
asasi ya Kukuza Utawala na Uwazi Tanzania (IGT), Edwin Soko alisema Rais
amefanya vizuri kufuta safari za nje na kwamba njia hiyo itamfanya
aweze kutimiza ahadi zake, kama kutoa Sh50 milioni kwa kila Kijiji,
kujenga barabra za kisasa pamoja na kununua meli mpya.
Ofisa
Ustawi wa Jamii, Mwanza, Davis Justine alisema Dk Magufuli amefanya
vizuri kuagiza wafanyabiashara wakubwa wabanwe na kulipaa kodi na kufuta
safari za nje, kwa kuwa zilikuwa zinapoteza fedha nyingi ambazo
zingewekezwa katika sehemu nyingine zingeleta maendeleo.
Sharon Sauwa, Lauden Mwambona, Lilian Lucas, Ngollo John, Peter Elias, Mussa Juma na Raymond Kaminyoge.
No comments:
Post a Comment