Dar es Salaam. Wakati makada wa CCM, wakionyesha nia ya
‘kimya kimya’ kuwania nafasi ya kiti cha Spika wa Bunge la 11, chama
hicho kimesema anayetaka nafasi hiyo ruksa kujipitisha kwa wabunge
kuomba kura.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC),
Idara ya Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatibu alisema jana kuwa
wanachama wake wanao uhuru wa kufanya maandalizi yao ya kujitangaza.
“Sisi bado hatujaanza rasmi lakini hatuwezi kuwazuia wanachama wanaotaka
nafasi hiyo kuanza kufanya ‘lobbying’ mapema... ni haki yao,” alisema.
Khatibu
alisema CCM kwa sasa hawajaanza kutoa fomu za kuwania nafasi hiyo kwa
wagombea wake hadi ofisi ya Bunge itakapotangaza rasmi kuwania nafasi
hiyo.
“Tunasubiri ofisi ya Spika wa Bunge watangaze
kwanza utaratibu wao na sisi ndiyo tutaanza kutoa fomu hizo na siwezi
kusema itakuwa lini,” alisema Dk Khatibu.
Hadi sasa
makada wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Samuel Sitta na Anne Makinda,
waliokalia kiti cha spika wa mabunge mawili yaliyopita.
Wengine
wanaotajwa kuwania kiti hicho, wabunge wateule, Mussa Hassan Zungu
(Ilala), Jenista Mhagama (Peramiho), George Simbachawene (Kibakwe) na
Job Ndugai (Kongwa).
Kikatiba, kiti cha spika kinaweza kuwaniwa na mtu yeyote ambaye atapitishwa na chama chake bila ya kujali kama ni mbunge.
Iwapo mgombea hatakuwa mbunge mteule, ni lazima jina lake lipitishwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakati
hali ikiwa haijapamba moto ndani ya CCM, Mwanasheria Mkuu wa Chadema,
Tundu Lissu jana alisema vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF havijaanza mikakati
ya kupitisha mtu atakayegombea uspika, badala yake vinaandaa kambi
imara ya upinzani kwa ajili ya kuibana Serikali bungeni.
Akizungumzia
utaratibu wa kumpata spika, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel
aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa wagombea wa nafasi hiyo
wanaruhusiwa kutoka vyama mbalimbali vya siasa.
Joel alisema mchakato wa kuwania nafasi hiyo utaanza baada ya Rais John Magufuli kuitisha Bunge.
“Nafasi
hii haigombewi na mgombea binafsi. Ni lazima apitishwe na chama. Kama
ni mbunge mteule jina lake linaletwa moja kwa moja katika ofisi za Bunge
ila kama ni mwanachama wa kawaida lazima athibitishwe na NEC kuona kama
ana sifa,” alisema Joel.
Alisema Rais akishaitisha
vikao vya Bunge, chombo hicho cha kutunga sheria ndiyo kitaanza mchakato
wa uchaguzi wa spika na kazi ya kwanza itakuwa kupokea majina ya
wagombea kutoka vyama mbalimbali.
No comments:
Post a Comment