Zanzibar. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad amesema yuko tayari kukamatwa na kufikishwa mahakamani
kujibu mashtaka, kama kitendo chake cha kujitangazia ushindi ni kosa.
Maalim
Seif alikuwa akizungumza na viongozi wa majimbo, makatibu wa matawi,
wajumbe wa mkutano mkuu, wajumbe wa kamati za utendaji za ngazi zote na
watendaji wa chama hicho.
Alisema haoni hatua yake ya
kuitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imtangaze kuwa mshindi haina
matatizo kwa kuwa ana uhakika kuwa ndiye aliyeshinda kwenye uchaguzi.
“Nilichosema ni ZEC initangaze kwa kuwa
nilishinda uchaguzi. Je, hapo kuna ubaya gani ati? Nishitakini basi,
nasema niko tayari, nishtakini. Nitakuja mahakamani kujitetea, mnamtisha
nani! Mnamtisha nani hapa?” alihoji.
Maalim Seif
aliwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF akiungwa mkono na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akichuana vikali na
mgombea wa CCM, Dk Mohamed Shein.
Hadi sasa, Tume ya
Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) haijamtangaza mshindi na badala yake
imefuta matokeo ya kura za nafasi hiyo pamoja na za uchaguzi wa
wawakilishi, ikisema uchaguzi utarudiwa tena ndani ya siku 90.
Hata hivyo, CUF imepinga ikitaka ZEC imtangaze mshindi kwa madai kuwa chama hicho ndicho kilichoibuka na ushindi.
Jana,
Maalim Seif, ambaye ameshagombea urais wa Zanzibar mara tano, alirudia
wito wake wa kuitaka ZEC imtangaze kuwa mshindi ili aapishwe na kuanza
kazi, ikidai anataka kuanza kuijenga upya Zanzibar. Pia alisisitiza
msimamo wake wa kushirikiana na CCM katika utawala wake kwa kuwa Katiba
ya Zanzibar inaelekeza chama kinachoshinda kuunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK).
“Sijui wenzetu wanachohofia ni nini na
mara hii sisi (CUF) tumeshinda viti 27 na wao idadi hiyo hiyo ya viti 27
vya Baraza la Wawakilishi, tutakuwa na idadi sawa kwa sawa ya mawaziri
tuongoze nchi pamoja,” alisema Maalim Seif.
Kiongozi huyo wa CUF alihoji sababu za Rais Shein kutokubali kushindwa akihoji anaona ubaya gani kuridhia.
“Tukae
pamoja tuunde Serikali akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais au kama hataki
CCM wamteue mtu yoyote tuongoze nchi. Mbona mimi niliridhia kuwa Makamu
wa Kwanza?” alihoji.
Maalim Seif alisema hakuna namna yoyote ya kupindua uamuzi wa wananchi walioufanya kupitia masanduku ya kura.
Alisema
wanachokifanya ZEC ni kuchelewesha kukamilisha uhakiki wa kura kwa
majimbo 14 yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa urais, na hivyo
kuishauri ZEC kukamilisha kazi ili serikali mpya ianze kufanya kazi ya
watumikia wananchi.
Alisema tayari dunia nzima
wanamfahamu rais aliyechaguliwa na wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi
Mkuu uliopita, na kuwataka wanachama wa CUF kuacha kusikiliza kile
alichokiita proganda za CCM zinazoeleza kurejewa kwa uchaguzi.
Akizungumzia
madai ya ongezeko la kura katika kisiwa cha Pemba, Maalim Seif alisema
hayo hayana ukweli kwani hakuna hata ‘kituo kimoja kilichozidishwa
wapiga kura 350 kama ZEC ilivyopanga, akisema vingine vilikuwa na
wapigakura chini ya idadi hiyo.
Mapema akizungumza
katika mkutano huo, mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa CUF, Omar Ali
Shehe alisema chama hicho kimepata ushindi mkubwa kwa nafasi za
uwakilishi na udiwani.
Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2010 chama hicho kilipata wawakilishi wanne na madiwani saba
kisiwani Unguja, lakini katika uchaguzi wa 2015 kimepata wawakilishi
tisa na madiwani 15.
Kiongozi huyo alisema CCM
imepoteza kata zote tatu za udiwani katika kisiwa cha Pemba na kukifanya
chama hicho kushindwa kupata mjumbe katika Baraza la Wawakilishi,
ubunge na udiwani.
Kabla ya mkutano huo, alielezea
kauli ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF kilichokutana chini ya
mwenyekiti wake, Twaha Taslima, akisema kiliishauri ZEC kutengua uamuzi
wa mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha wa kufuta uchaguzi mkuu wa
Zanzibar, kwa vile hana mamlaka ya kikatiba na wala Sheria ya Uchaguzi
ya Zanzibar hampi nguvu ya kufuta uchaguzi huo.
Jecha amekuwa akidaiwa kufanya uamuzi huo bila ya kushirikisha viongozi wenzake wa ZEC.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, matokeo ya uchaguzi wa Rais
yanatakiwa kutolewa siku tatu baada ya wananchi kupiga kura na yanaweza
kucheleweshwa kwa siku tatu zaidi iwapo kutatokea matatizo katika
kuhesabu kura.
No comments:
Post a Comment