Wakati
Jumuiya za kimataifa zikiendelea kushinikiza mgogoro wa kisiasa
Zanzibar umalizwe, wawakilishi wateule 27 wa CUF Zanzibar, wamepigilia
msumari wakisema wao ni wawakilishi halali na kwamba hawatambui kufutwa
kwa uchaguzi wa Zanzibar.
Wawakilishi
hao wamesema kuwa, sheria na Katiba ya Zanzibar haziruhusu mtu yeyote
kufuta matokeo yao, kwa kuwa walishatangazwa na kupewa vyeti vya
ushindi.
Wawakilishi
hao 18 kutoka Pemba na tisa kutoka Unguja ambao ni kati ya wawakilishi
54 wa majimbo yote ya uchaguzi visiwani humo, waliyasema hayo jana
jijini Dar es Salaam.
Akisoma
tamko kwa niaba ya wenzake, Mwakilishi wa Mgogogni, Abubakar Khamis
Bakari alisema wawakilishi wote walishapigiwa kura, kutangazwa na kupewa
vyeti vya kutambuliwa kwa ushindi wao na hakuna mtu yoyote
aliyelalamika kuwa uchaguzi ulikuwa na dosari.
“Ni
kutokana na kukamilika kwa hatua zote bila kuwepo malalamiko yoyote na
kwa kufuata masharti ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi ya
Zanzibar namba 11 ya mwaka 1984, ndipo wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo
yote ya Unguja na Pemba wakatutangaza washindi wa nafasi za uwakilishi
na udiwani na pia kutupa taarifa za maandishi wagombea tulioshinda,” alisema bakari ambaye katika Serikali iliyopita alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Alisema
kifungu hicho cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kinaeleza
kuhusu mamlaka ya msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo.
Alinukuu kifungu kidogo (a) kinachosema. “Haraka
atamtangaza mgombea aliyepata wingi wa kura halali zilizopigwa kuwa
amechaguliwa; na (b) atapeleka taarifa ya maandishi kwa mgombea
aliyeshinda; na (c), atatoa taarifa ya matokeo ya uchaguzi kwa tume
ambayo itapeleka matokeo hayo, pamoja na idadi ya kura alizopata kila
mgombea katika kila jimbo kutangazwa katika gazeti rasmi,” alisema.
Alisema,
Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 11 ya mwaka 1984, imetoa uwezo na
mamlaka yote ya kusimamia na kuendesha uchaguzi wa wawakilishi na
madiwani kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo.
Alisema
hakuna sehemu yoyote katika Katiba ya Zanzibar ya 1984 wala katika
Sheria ya Uchaguzi inayotoa uwezo au mamlaka kwa Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar kwa ujumla wake, kufuta uamuzi wa msimamizi wa
uchaguzi wa wawakilishi na madiwani.
Alisema
kazi pekee iliyotajwa katika kifungu cha 88 (c), cha sheria ya uchaguzi
ni kwa tume ya uchaguzi baada ya kupokea taarifa ya matokeo ya uchaguzi
kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo na idadi ya kura alizopata
kila mgombea katika kila jimbo, kutangaza matokeo hayo katika gazeti la
serikali.
“Sheria
ya Uchaguzi ya Zanzibar, kifungu cha 123, kimeweka bayana kwamba baada
ya msimamizi wa uchaguzi kumtangaza mshindi, nafasi pekee ya mtu mwenye
malalamiko kutaka matokeo hayo yatenguliwe ni kwa kufungua kesi ya
kupinga matokeo ya uchaguzi katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.
“Kwa
hiyo si mwenyekiti wa tume wala tume yenyewe mwenye uwezo wa kutengua
matokeo ya uchaguzi ya mwakilishi au diwani yaliyokwisha tangazwa na
msimamizi wa uchaguzi. Uwezo na mamlaka hayo yamewekwa kwa Mahakama Kuu
ya Zanzibar pekee,” alisema.
Bakari
aliitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kufuta uamuzi wa
mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha na kuendelea na majumuisho ya kura za
rais na kumtangaza mshindi.
Alisema ni vema wawakilishi wote kutoka vyama vyote, wakaapishwa ili waanze kuwatumikia wananchi.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mtopepo, Nassor Ahmed Mazrui,
alikanusha taarifa kuhusu mgombea urais wa chama hicho Zanzibar, Maalim
Seif Sharif Hamad, kukutana na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis
Mamunyange kama ilivyopendekezwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Mazrui
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar) aliulizwa iwapo
kuzungumza kwao na waandishi wa habari, kunatoka na mazungumzo ya Rais
mstaafu Kikwete na Maalim Seif kutozaa matunda.
“Maalim
Seif ataendelea kufanya mazungunzo na watu wa ngazi yake na sisi
tutaendelea kusema yetu, sisi hapa leo tumekuja na suala la wawakilishi,” alisema Bakari.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa chama
hicho, Jussa Ismail Ladhu, alisema inashangaza kuona uchaguzi wa
wawakilishi kubatilishwa hali ya kuwa ule wa wabunge wa Muungano
ukionekana ni halali.
“Uchaguzi
huo ulifanywa kupitia daftari moja la wapiga kura, kitambulisho kimoja.
Hicho hicho ndiyo kilitumika kupiga kura tano ikiwa ni pamoja na za
wabunge wa Zanzibar, wawakilishi, madiwani na wabunge wa Bunge la
Muungano,” alisema Jussa ambaye ni Mwakilishi mteule wa Jimbo la Malindi.
Novemba
5, mwaka huu aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alisema CUF inaendelea
kutafuta haki ya Wazanzibari kutaka ZEC iendelee kutangaza matokeo ya
uchaguzi, ili mshindi ajulikane na hatimaye kuapishwa.
Aliyasema
hayo wakati akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika makao makuu ya
CUF Mtendeni, baada ya kurejea visiwani humo katika safari yake ambayo
alikutana na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Fatma Karume Apinga
Katika
kile kinachooneka kuibuka kwa mgogoro wa kikatiba, Mwanasheria wa
visiwani Zanzibar Fatma Karume, hivi karibuni, alisema Mwenyekiti wa ZEC
amevunja Katiba ya Zanzibar akisema uamuzi wa kufuta uchaguzi ni wake
binafsi na si tamko la kisheria.
“Tuseme
ukweli si Jecha, kwa sababu Jecha hana jeshi. Jecha hana Polisi.
Wazanzibari tumenyimwa haki yetu si na Jecha. Tumenyimwa haki yetu na
wale watu waliotuma Jeshi pale na kutuma polisi pale,” alisema Fatma.
Akizungumza
katika mahojiano na Redio Ujerumani (DW), Fatma, aliwatupia lawama
wenye mamlaka na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Polisi, kwa kuzuia
kutangazwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar.
“Kama
ni kusema, Jecha kasema tu, lakini hana mamlaka na kama ni kulaumiwa
Jecha atalaumiwa kwa kutumiwa dhidi ya masilahi na haki ya Wazanzibari,” alisema.
Akizungumzia
suala hilo kikatiba na kisheria, Fatma Karume alisema Serikali imezuia
kutangazwa matokeo ya uchaguzi na wala si kufuta uchaguzi, kwa sababu si
Jecha wala serikali iliyo na mamlaka ya kufuta uchaguzi.
Mawaziri waachia ngazi
Wakati
hali ikiendelea hivyo, juzi mawaziri sita kutoka chama cha CUF waliopo
katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo walitangaza kuacha
ngazi kwa kile walichodai kuwa ni kumalizika kwa muda wa serikali hiyo
inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein.
Akitoa
taarifa hiyo juzi visiwani Zanzibar katika kikao cha Baraza Kuu la
Uongozi la chama hicho, Bakari alisema mawaziri wote wa chama hicho
pamoja na manaibu watatu wamekwisharudisha magari ya Serikali katika
mamlaka husika.
Bakari
alisema kwa mujibu wa kifungu cha 28 (2) cha Katiba ya Zanzibar kipindi
cha Dk. Shein pamoja na baraza la mawaziri kuendelea kubaki madarakani
kimekwisha tangu Novemba 2, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment