Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Mohamed Shein na mwenzake wa ya CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad jana walikutana kwa faragha kwa takriban saa tano, lakini hakuna taarifa iliyotolewa kuhusu kilichojadiliwa kwenye kikao hicho.
Kikao hicho, ambacho pia
kiliwahusisha marais wastaafu wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano, Ali
Hassan Mwinyi na Amani Karume, kimefanyika katika kipindi ambacho kuna
hali ya sintofahamu visiwani hapa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha atangaze kufuta matokeo ya uchaguzi wa
Rais na wawakilishi.
Jecha, ambaye alifuta matokeo hayo siku
chache baada ya Maalim Seif kujitangazia ushindi, aliahidi kuitisha
uchaguzi mpya ndani ya siku 90, lakini CUF imesema haitashiriki.
Kikao kilichofanyika Ikulu ya Mnazi Mmoja mjini hapa, kilianza saa 4.15 asubuhi na kumalizika saa 9.40 mchana.
“Ikulu
ilikuwa tulivu hakuna kilichoonekana kuongeza harakati licha ya vizuizi
vya kamba vilivyokuwa vimezungushwa tangu ulipomalizika uchaguzi,”
alisema mmoja wa maofisa watendaji wa ofisi hiyo ya Rais.
Hii si
mara ya kwanza kwa wawili hao kukutana tangu kumalizika kwa uchaguzi
ulioiweka Zanzibar njia panda baada ya ZEC kuamua kutoendelea kutangaza
matokeo.
Hata hivyo, inaonekana ni mara ya kwanza kwa wagombea hao
kukaa meza moja na safu kubwa ya viongozi hao wa kisiasa na maongezi
yao kuchukua muda mrefu.
Mkutano huo umefanyika siku moja baada ya
Maalim Seif kukutana na watendaji wa kamati za utendaji za matawi na
wilaya wa Unguja na pia jana kuongea na viongozi wa ngazi hizo kwa
upande wa Pemba.
Katika vikao hivyo, Maalim Seif amekuwa akisisitiza wafuasi kuendelea kuwa watulivu huku akiahidi kuendelea kupigania haki yake.
No comments:
Post a Comment