Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Doroth Msuya, mkazi wa Monduli mkoani Arusha, ametoweka muda mfupi kabla ya kufunga ndoa na Joseph Machange, mkazi wa Mwika, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ndoa
ya wawili hao ilitarajiwa kufungwa Jumamosi ya Novemba 7 katika Kanisa
la Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Usharika
wa Lole, Mwika.
Mchungaji
mwenza wa usharika huo, Elikeseni Shao, alisema majira ya saa sita na
nusu mchana wakati maandalizi ya ibada ya ndoa yakiwa yamekamilika,
walipokea taarifa za kutoweka kwa bibi harusi huyo akiwa saluni.
“Sisi
kama viongozi wa kanisa tulipokea kwa masikitiko taarifa za kutoweka
kwa aliyekuwa bibi harusi mtarajiwa wakati akiwa saluni, na kwamba
liliwashtua sana ikizingatiwa kuwa maandalizi yote ya ndoa yalikwisha
kamilika na kumuacha bwana harusi solemba,” alisema.
Alisema
uongozi wa kanisa hilo baada ya kupewa taarifa hizo iliwalazimu
kuitisha kikao cha familia zote mbili na kuzungumza nao juu ya tukio
hilo ambapo pia walichukua hatua ya kuzifanyia maombi familia hizo ili
zisiingie katika mawazo ya imani za kishirikina.
Akielezea
mazingira ya tukio hilo, mmiliki wa saluni aliyokuwa akipambiwa bibi
harusi, Stella Mringo, alisema awali alimpokea mteja huyo saa nne
asubuhi na ilipofika saa sita na nusu mchana alimuomba amruhusu atoke
kwenda kujisaidia.
Alisema bibi harusi huyo alitoka nje akiwa na mpambe wa watoto aliyefahamika kwa jina moja la Esther.
“Lakini mpambe huyo alirudi na kuchukua khanga ya bibi harusi na alipotoka tena hakumkuta,” alisema.
Kwa
upande wake, mshereheshaji wa sherehe hiyo, William Ngalo, alisema
akiwa kwenye ukumbi wa sherehe uitwao Mamba Complex, alipokea taarifa
kuwa asiendelee na kazi ya kufunga muziki kwa kuwa kuna matatizo
yamejitokeza, na alipofuatilia alijulishwa kuwa bibi harusi alitoweka
katika mazingira ya kutatanisha.
Alisema
bibi harusi huyo alitafutwa eneo lote la Mwika bila kupatikana jambo
lililolazimu chakula kilichoandaliwa katika sherehe hiyo kuliwa nyumbani
kwa wazazi wa bwana harusi majira ya saa tatu usiku.
Kwa
upande wake, baba wa bwana harusi mtarajiwa, Eliringia Machange,
alisema wao kama familia wamepokea kwa masikitiko tukio hilo na kwa sasa
hawawezi kusema chochote.
Bwana
harusi mtarajiwa, Joseph Machange, alisema jambo lililomtokea haliamini
kwani limemuumiza, hasa baada ya kutumia fedha zaidi ya milioni saba
kwa ajili ya maandalizi ya harusi hiyo.
Alisema kwa sasa suala hilo limeripotiwa katika kituo kidogo cha polisi Himo, na kwamba wanasubiri uchunguzi uendelee.
No comments:
Post a Comment