Wabunge wa mkoa wa Dodoma wamejipanga kuwasilisha hoja binafsi bungeni ya kuitaka serikali kuhamia mkoani humo na utungwaji wa sheria ya kuutambua rasmi kuwa ni makao makuu ya nchi, kutokana na utekelezwaji wake kusuasua.
Wabunge
hao walisema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao chao cha pamoja na
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), ambacho lengo lake
lilikuwa kujenga hoja za pamoja katika kuishawishi serikali kuhamia
mkaoni hapa.
Kikao
hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Dodoma, Adam Kimbisa na wabunge hao waliazimia kushirikiana ili suala
hilo likubalike na kutekelezwa.
Mbunge
wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (CCM), alisema pamoja na jitihada hizo
ni vyema CDA ikajiangalia upya katika utekelezaji wa majukumu yake ili
kusiwapo na msuguano na wananchi.
Aliitaka
CDA kuangalia upya gharama za upimaji wa viwanja ambazo asilimia kubwa
ya wananchi wa kipato cha chini wanashindwa kuzimudu.
“Kama
kuna maeneo ya kurekebisha, yarekebishwe sasa ili kuendana na kasi ya
kuitaka serikali ihamie Dodoma ikiwa ni pamoja na gharama hizo
kupunguzwa. Gharama ya chini ya upimaji kiwanja kwa sasa inaanzia Sh.
500,000 kiasi ambacho wanashindwa kukimudu.
Naye
Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM), alisema mpango wa
serikali kuhamia Dodoma upo, lakini umekuwa ukisuasua, hivyo inatakiwa
nguvu mpya ya kulisukuma jambo hilo ili litekelezwe.
“Kwa
muda mfupi iangaliwe namna CDA na Manispaa ya Dodoma zinavyoweza
kushirikiana katika majukumu yao kutokana na kuwapo kwa mgongano wa
kisheria juu ya uundwaji wa mamlaka hiyo na manispaa,” alisema.
Simbachawene
aliitaka mamlaka hiyo kufanya kazi kwa karibu na wanasiasa ili
kurahisisha ufikishaji wa elimu kwa wananchi na kuondoa malalamiko.
“CDA
imefanya kazi katika mazingira magumu, lakini imesaidia Dodoma
kuonekana mji wa tofauti kwani umepangika vizuri sana, kuna vitu
vichache vya kurekebisha ili isionekane kama ni shetani (kero) kwa
wananchi wa Dodoma,” alisema Simbachawene.
Naye
Mbunge wa Kondoa Vijijini, Dk. Ashatu Kijaji (CCM), alisema yupo tayari
kushirikiana nje na ndani ya Bunge ili Dodoma ifikie matarajio yake.
Mbunge
wa Viti Maalum (CCM), Felista Burra, alisema suala la serikali kuhamia
Dodoma limekuwa likiwekewa mikakati, lakini limekuwa likikosa watu wenye
dhamira ya dhati kulisukuma ili litekelezwe.
Alisema
mchakato huo umekuwa ukikwamishwa na serikali, lakini anaamini hoja
hiyo ikiwasilishwa bungeni wabunge wengi watasaidia utekelezaji wake
ukamilike.
Kwa
upande wake, Kimbisa alisema viongozi wa Dodoma wamekuwa wakilaumiwa na
wananchi kwa kushindwa kuibana serikali ihamie mkoani hapa.
Alisema kilio cha watu wa Dodoma ni kuona inakuwa makao makuu ya nchi kama ilivyokwisha tangazwa na serikali.
“Wabunge
mnategemewa sana kufanikisha jambo hili, kwani ndiyo mliopewa dhamana,
maana hakuna mtu nje ya Bunge atakayeweza kufanikisha,” alisema Kimbisa.
No comments:
Post a Comment