Vifaru na Magari ya Maji ya Kuwasha Havitaleta Ufumbuzi Wa Mgogoro Zanzibar-CUF - LEKULE

Breaking

2 Nov 2015

Vifaru na Magari ya Maji ya Kuwasha Havitaleta Ufumbuzi Wa Mgogoro Zanzibar-CUF

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar hauwezi kupatikana kwa kutumia nguvu au vitisho vya kuingiza vifaru na magari ya maji ya kuwasha, kama inavyotokea sasa; bali kinachotakiwa ni meza ya majadiliano.
 
Tamko hilo limetolewa na mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
 
Aliwataka wafuasi wa CUF na wananchi kuendelea kuwa na subira wakati viongozi wao wakiwa katika jitihada za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
 
Alisema mgogoro uliojitokeza Zanzibar ni mgogoro wa kisiasa baada ya haki ya kidemokrasia ya wananchi kupindishwa ndio maana CUF inataka Mwenyekiti afute uamuzi wake, amalizie kazi iliyobakia ya kuhakiki matokeo na kutangaza mshindi.
 
"Tatizo lililopo ni la kisiasa na ufumbuzi wake si vifaru wala kuongeza ulinzi, linahitaji njia ya mazungumzo kumalizika kwake," alisema.
 
Aidha, Maalim Seif aliwataka wanachama kuendelea na utulivu kutokana na juhudi zinazofanywa na Jumuiya za Kimataifa kuonesha mwelekeo wa kupatikana ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.
 
Alisema CUF inaimani kwamba ufumbuzi wa haki wa suala hilo hauko mbali na Wazanzibari wataona mafanikio ya demokrasia yatakayojengwa nchini. Alisema haki lazima itendeke katika uchaguzi uliopita.
 
"Sisi tumepata moyo na imani kwamba ufumbuzi wa haki wa suala hili hauko mbali na Wazanzibari wataona mafanikio ya demokrasia yetu tunayoijenga katika nchi yetu," alisisitiza Maalim Seif.
 
Aliwaomba Wazanzibari wote wanaopenda amani wawe waangalifu sana na taarifa za uongo zinazotolewa za kuchochea kufanya vurugu kwa kisingizio kuwa zimetolewa na viongozi wa CUF wakati ni uongo.
 
"Nitumie fursa hii kuwashukuru wale wote wanaofanya juhudi kubwa kuona ufumbuzi wa haki na wa amani unapatikana kwa tatizo hili lililosababishwa na mtu mmoja aliyeamua kuacha wajibu wake na kutumikia maagizo ya kikundi cha watu wabinafsi", alisema.
 
Aidha, alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, bado wana nafasi kubwa ya kuhakikisha wanaivusha Zanzibar kwa kumaliza mgogoro wa uchaguzi uliojitokeza kwa amani na utulivu.
 
"Kwa mara nyingine tena natoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Dkt Shein kuchukua dhamana ya uongozi na kwa pamoja tushirikiane kuikwamua Zanzibar na Tanzania katika mkwamo huu", alisema.
 
Alisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vina wajibu mkubwa wa kusaidia kupatikana ufumbuzi wa tatizo walilonalo badala ya kuongeza wasiwasi kwa wananchi wao waliotulia.
 
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar, alisema kuwa wamepata taarifa kuwa Mwenyekiti huyo ameitisha kikao cha Tume na kuwataka makamishna kuunga mkono uamuzi wake huo alioutangaza pekee wa kufuta matokeo ya uchaguzi.
 
Alisema kuwa ni vyema kwa Mwenyekiti huyo akatambua kwamba hata akiwatumia baadhi ya makamishna kumuunga mkono, bado uamuzi huo hautakuwa halali kwa sababu haumo katika uwezo uliopewa Tume; si katiba wala sheria ya uchaguzi.
 
"Kwa ufupi suala hili halina njia nyingine ya kulimaliza zaidi ya kukamilisha kazi ya kufanya majumuisho, kuhakiki matokeo na kumtangaza mshindi wa uchaguzi", alisema Maalim Seif.
 
Maalim Seif aliwahakikishia viongozi na wanachama wa CCM kwamba hawana sababu ya kuwa na hofu na maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya Oktoba 25 mwaka huu; na kwamba kama kuna tofauti zozote za kisera na kimtazamo baina yao zinaweza kuzungumzwa na maelewano kufikiwa.
 

"Nawahakikishia viongozi na wanachama wa CCM na Wazanzibari wote kwamba hakutakuwa na ulipizaji kisasi au kufukua makaburi kwa mambo yaliyopita, sote tutafanya kazi pamoja bila ya kujali tofauti za itikadi za kisiasa, asili, kabila au dini zetu, Zanzibar ni moja na itabaki kuwa moja," alisisitiza Maalim Seif. 

No comments: