Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetoa tamko kuwa Rais wa Zanzibar, Dkt.
Ali Mohamed Shein, ataendelea kushikilia wadhifa huo hadi hapo rais
mwingine atakapochaguliwa kihalali na kuapishwa.
Akitoa
taarifa ya Serikali kwa vyombo vya habari mjini hapa jana, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed, alisema
Katiba ya Zanzibar inamruhusu kuendelea na wadhifa huo hadi hapo
atakapoapishwa Rais mwingine.
"Tunapenda
kuwataarifu wananchi kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 28 (1) (a) cha
Katiba ya Zanzibar ya 1984 kinaweka sharti la kwamba mtu ataendelea kuwa
Rais hadi Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais," alisema na kuongeza;
"Hivyo
kwa kuzingatia maelekezo hayo ya Katiba, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
inayoongozwa na Dkt. Ali Mohamed Shein, ipo na itaendelea kuwepo hadi
hapo uchaguzi utakapokamilika na Rais atakayechaguliwa kula kiapo."
Mohamed
alisema ni vizuri wananchi wakaelewa Rais wa Zanzibar anachaguliwa kwa
mujibu wa kifungu cha 27 cha Katiba ya Zanzibar na sheria ya uchaguzi
namba 11 ya 1984 ambayo imeweka utaratibu wa matokeo ya uchaguzi huo.
Sheria
ya uchaguzi kifungu cha 42 (4) kinaeleza kuwa mgombea nafasi ya urais
atatangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar baada ya kupata kura nyingi za
halali.
Aidha,
kifungu cha 42 (5) cha sheria ya uchaguzi kinakataza kwa mtu au taasisi
yoyote kutangaza matokeo ya uchaguzi kinyume na sheria ya uchaguzi; na
ni kosa la jinai kufanya hivyo."
"Serikali
haitamvumilia mtu yeyote atakayekiuka sheria na atashughulikiwa kwa
mujibu wa sheria. Na kwa taarifa hii, Serikali inaviagiza vyombo vya
ulinzi na usalama kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa wale wote
walioanza kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani. Ni vizuri wananchi
waendelee kuwa watulivu na kusikiliza taarifa za Serikali" alisema Aboud.
No comments:
Post a Comment