Meneja
Mradi Ruvu chini Mhandisi Emmanuel Makasa akiwaonesha waandishi wa
habari sehemu ya bomba la kusafirisha maji kutoka chanzo cha Ruvu chini
kwenda jijini Dar es salaam.
Sehemu
ya bomba la kusafirisha maji kutoka chanzo cha Ruvu chini kwenda jijini
Dar es salaam lilivyozamishwa chini tayari kwa kusafirisha maji ambayo
yatawanufaisha wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kwa matumizi
mbalimbali.
Baadhi ya mitambo ya kusafisha maji ambayo yamesafishwa tayari kwa matumizi ya wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani.
Baadhi ya waandishi wa habari na viongozi kutoka Wizara ya Maji wakiwa eneo la chanzo cha maji cha Ruvu Chini.
Baadhi
ya waandishi wa habari na viongozi kutoka Wizara ya Maji wakiwa eneo la
chanzo cha maji cha Ruvu Chini wakipita juu ya eneo la kusafisha maji
kabla ya kusafirishwa kwa matumizi mbalimbali.
Meneja
Mradi Ruvu chini Mhandisi Emmanuel Makasa (aliyevaa tai) akiongea na
waandishi wa habari walipotembelea ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu
Chini kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Dar es salaam.
Fundi
akiendelea na kazi ya kuunganisha na kuchomelea bomba la maji ambalo
litasafirisha maji kutoka Ruvu Chini kwenda jijini Dar es salaam.
Muonekano wa maji yakiwa mtoni kabla ya kuanza kusafishwa kupitia hatua mbalimbali kwa matumizi.
(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Mamlaka
ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea kuboresha
na kuimarisha miundombinu ya maji ili kuwanufaisha wakazi wa mikoa ya
Dar es salaam na Pwani kupata maji kwa mahitaji yao ya kila siku.
Mioundombinu
hiyo inayoboreshwa ni pamoja na bomba la Ruvu Chini lenye urefu wa
Jumla ya km 55 ambapo hadi sasa km 52.6 zimekamilika na zimebaki km 2.4
ili kukamilisha mradi huo ambao utasaidia kusimamia moja ya sentensi ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
ya “Kuwatua akina mama ndoo za maji kichwani”
Ili
kufikia azma hiyo ya kuwapatia maji safi na salama wakazi wa mikoa hiyo,
Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang'ingo alisema
kuwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini na ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu
Chini hadi matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi ndiyo utakuwa suluhisho la
tatizo la maji katika jiji la Dar es salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani.
Akiongea
na waandishi wa habari ofisini kwake kabla ya waandishi hao kwenda
kujionea hatua iliyofikiwa, Mwang'ingo alisema kuwa ujenzi wa mradi huo
unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2016 na kuondoa adha ya maji
kwa wananchi na kuwaunganishia wengine ambao hawakuwa na huduma ya maji.
“Tumelazimika
kufikia hatua ya kupanua huduma ya upatikanaji wa maji katika mikoa ya
Dar es salaa na Pwani kutokana na ongezeko la watu kulingana na sensa ya
watu ya mwaka 2012, mkoa wa Dar es salaam una jumla ya zaidi ya watu
milioni 5 ambao watatumia maji zaidi ya lita milioni 5 kwa siku”,
“Katika
upanuzi huo, kumekuwa na changamoto ya makazi ya watu kuwa ndani ya
mradi ambapo kulikuwa na kesi 17 katika mahakama mbalimbali katika
maeneo hayo ikiwemo mahakama ya ardhi, hadi sasa DAWASA imeshinda kesi
13 na kupewa haki ya kutumia njia hiyo kukamilisha upanuzi wa mradi”
alisema Mwang'ingo.
Kwa mujibu wa Mwang'ing'o kesi nne bado zipo mahamani na ambazo zimefikia hatua mbalimbali kulingana na taratibu za kimahakama.
Lengo
la mradi huu ni kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 182 hadi
270 kwa siku. Mradi ambapo awamu itakayofuata ni lita milioni 360 kwa
siku.
Chanzo
cha maji cha Ruvu Chini ndiyo chenye kiwango kikubwa ambacho kina
wapatia maji wakazi wa Dar es salaam kwa zaidi ya asilimia 75
ikilinganishwa na asilimia 25 kutoka Ruvu Juu.
Mradi
wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini unalenga kuongeza uzalishaji maji na
kuwahudumia wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ) Bagamoyo, Chasimba,
Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani
Maeneo
mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar es salaam ni
Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo,
Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza, kijitonyama,
Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo, Vingunguti, Buguruni, Kariakoo na
Ilala.
No comments:
Post a Comment