Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM Awataka Wananchi Kutomchagua Lowassa Kwa Sababu ni GOIGOI - LEKULE

Breaking

23 Oct 2015

Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM Awataka Wananchi Kutomchagua Lowassa Kwa Sababu ni GOIGOI


MGOMBEA Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Hassan Suluhu amewaonya wananchi kutochagua upinzani kwani mgombea wao ni goigoi na anaweza kuunda serikali goigoi.

“Nawaombeni wana Iringa msichague watu wa upinzani ni goigoi na rais goigoi ataunda serikali goigoi na serikali goigodi italeta maendeleo goigoi,” alisema Samia alipohutubia wananchi mkoani Iringa wiki hii.

Aliwahakikishia wananchi wa Iringa kuwa Serikali ijayo ya Dk John Magufuli endapo itaingia madarakani itatatua changamoto zinazowakabili kwani haitakuwa goigoi.

Pia, aliwahakikishia wananchi wa Mufindi Kusini kuwa waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha karatasi cha SPM Mgololo watalipwa fidia zao kwani tatizo hilo limekuwa la muda mrefu.

Akizungumza jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini hapa, aliwahakikishia kuwa Serikali ya Dk Magufuli ni ya kutumikia wananchi wote na kuwataka wananchi kujitokeza kupiga kura na baada ya kufanya hivyo warudi nyumbani.

“Napenda kuwahakikishia Dk Magufuli yupo kutumikia kila Mtanzania, hivyo mkichagua Serikali goigoi haiwezi kuwaletea maendeleo,” alisema.

Samia Suluhu aliwahakikishia wananchi wa Iringa Mjini kuwa ataboresha hospitali, elimu pamoja na kutatua changamoto iliyopo kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akiwa Mufindi Kusini, mgombea huyo mwenza alimhakikishia mgombea ubunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, Mendrad Kigola kuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho watalipwa fidia ili waondokane na makali ya maisha.

Wafanyakazi 710 ambao waliachishwa kazi mwaka 2005 baada ya kiwanda cha karatasi cha SPM Mgololo kubinafsishwa, bado wanaidai serikali kiasi cha Sh bilioni 3.7. Samia alisema watahakikisha wanalifanyia kazi mapema suala hilo mapema iwezekanavyo ili kumaliza tatizo hilo.


“Tunafahamu hili tatizo la fidia ni la muda mrefu, tunaahidi kulipatia ufumbuzi,” alisema.

No comments: