Baadhi
ya Wanachama wa CCM wa Majimbo ya Kiembe Samaki na Chukwani wakiwa
katika mkutano wa Kampeni wa Kuwanadi Wagombea nafasi za Ubunge,
Uwakilishi na Udiwani wa Majimbo hayo uliohutubiwa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Kampeni ya CCM Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Balozi
Seif akimnadi Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kiembe Samaki
kupitia Chama cha Mapinduzi Nd. Ibrahin Raza kwenye uwanja wa michezo
hapo Kiembe Samaki Wilaya ya Magharibi “B”.
Balozi
Seif akimnadi Mgombea nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia
Chama cha Mapinduzi Jimbo la Kiembe Samaki Mh. Mahmoud Thabit Kombo.
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif akimuombea kura Bibi Mwanaasha
Khamis Juma anayewania nafasi ya Uwakilishi kwa tiketi ya CCM Jimbo la
Chukwani Bibi Mwanaasha Khamis Juma kwenye Mkutano wa Kampeni
zinazoendelea ndani ya Majimbo hayo.
Balozi
Seif akiwanadi wagombe wa nafasi za Udiwani katika wadi zote zilizomo
ndani ya Majimbo la Kiembe Samaki na Chukwani hapo Uwanja wa Michezo wa
Kiembe Samaki.
Wagombea
nafasi hizo za Udiwani wa kwanza kulia ya Balozi Seif ni Nd. Maabada
Ali Wadi ya Mbweni, Ndugu Maulidi Mwinyi Mzee Wadi ya Mombasa, Nd.
Suleiman Muusa Wadi ya Shakani na Nd. Khamis Abdillah Wadi ya Kisauni.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kampeni ya Uchaguzi ya CCM Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema kwamba endapo CCM itaendelea kushinda tena kwenye uchaguzi Mkuu
wa mwaka huu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha kwamba
inafuta waraka zote za umiliki wa ardhi zilizochukuliwa kihadaa kwa sura
ya uwekezaji.
Alisema
wapo baadhi ya watu waliopewa dhamana na Serikali katika kusimamia
masuala ya ardhi na wakaamua kutumia vibaya madaraka yao kwa
kujilimbikizia maeneo ya ardhi kwa maslahi yao binafsi.
Balozi
Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati akiwanadi wagombea nafasi mbali
mbali za Uongozi katika Majimbo Mawili ya Kiembe Samaki na Chukwani
kwenye Mkutano wa Kampeni zinazowendelea Nchini uliofanyika katika
uwanja wa michezo wa Kiembe Samaki Wilaya ya Magharibi “ B ”.
Alisema
tamaa ya watu hao kujilimbikizia maeneo makubwa ya ardhi imechangia
kuikosesha mapato Serikali kuu kwa kipindi kirefu jambo ambalo upo
uwezekano wa maeneo hayo kupewa wawekezaji wenye nia thabiti ya kutaka
kuisaidia Nchi Kiuchumi.
Akizungumzia
siasa za Kampeni zinazoendelea Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM Taifa alisema uwezo wa upinzani wa kudhania kwamba
utaking’oa madarakani Chama cha Mapinduzi ni wa kujifurahisha na hatma
yake itaishia kuwadanganya wanachama pamoja na wafuasi wao.
Alisema
Upinzani utawezaje kuliongoza Taifa wakati viongozi wake wamo ndani ya
maamuzi yanayofanywa na Serikali katika Vikao vya Baraza la Wawakilishi
na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tokea kuanza kwa mfumo wa
Vyama vingi vya Siasa Nchini Tanzania kwa takriban Miaka 25 sasa.
Alisema
nguvu za Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza Sera na Ilani yake
iliyofikia zaidi ya asilimia 90% katika kipindi cha Mwaka 2010 hadi 2015
ndio kigezo sahihi kinachotoa ishara kwamba Chama hicho kitaendelea
kuungwa mkono na Wananchi walio wengi Tanzania Bara na Zanzibar.
Balozi
Seif alijinasibu kwa kuelezea kuwa tabia ya Viongozi na wafuasi wa
vyama vya upinzani kuendelea kumlalamikia kila mara hasa kwenye mikutano
yao ni dalili za wafuasi hao kuiogopa CCM kutokana na jitihada zake za
kuzisimamia Serikali zote mbili katika utekelezaji wa Ilani na sera
zake.
Akisisitiza
umuhimu wa suala la Amani Nchini hasa katika kipindi hichi cha mpito
kuelekea uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwezi huu Balozi
Seif amnbae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali
kamwe haitokubali kuona Nchi inaelekezwa katika kutiwa kwenye matatizo.
Balozi
Seif alitahadharisha na kuwashauri wale watu waliozoea shari, fujo na
mchafuko ni vyema wakafanya utaratibu wa kuelekea kwenye nchi zenye
vitendo hivyo na sio haa Zanzibar.
Mapema
Muasisi wa Jimbo la Chukwani Mzee Ali Hassan Khamis aliwanasihi
Wanasiasa hasa wale wa vyama vya upinzani kuacha kutengeneza fitna mbaya
na shari kwa kuwahusisha vijana wa Jimbo hilo ambayo kuachiliwa
kupaliliwa kwake inaweza kuleta hatari kwa hatma ya vizazi hivyo.
Mzee
Ali Hassan alisema Wazee na Wananchi wa Jimbo la Chukwani hawana nia
mbaya na viongozi wa Upinzani lakini tabia ya wanasiasa wake ya kupita
nyumba hadi nyumba kushawishi pamoja na kuhonga watu ni mwanmzo wa
ishara mbaya ya kutaka kuleta fujo na vurugu.
Naye
Mbunge Mstaafu wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mh. Ummy Aley
aliitanabahisha jamii kuwa na hadhari dhidi ya Viongozi wa Vyama vya
Upinzani walioamua tumia fedha za Umma kujinufaisha wao binafsi.
Mh.
Ummy alisema Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na
Wale wa Baraza la Wawakilishi wa Chama cha Wananchi CUF wametumia karibu
shilingi Bilioni 25 katika kipindi cha miaka Mitano na Shilingi Bilioni
Mia 100 katika kipindi cha miaka 20 tokea kuanza kwa mfumo wa vyama
vingi vya siasa.
Katika
Mkutano huo ulishirikisha Wanachama vindakindaki wa Majimbo ya Kiembe
Samaki na Chukwani Balozi Seif aliwaombea kura kwa Wananchi na Wana CCM
wagombea wote wa chama cha Mapinduzi wakati utakapowadia.
Wagombea
hao ni Ibrahim Raza Hassananali Ubunge Jimbo la Kiembe Samaki, Mahomud
Thabit Kombo Uwakilishi Jimbo hilo la Kiembe Samaki, Bibi Mwanaasha
Khamis Juma Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Chukwani, Nd.
Maabad Ali Udiwani Wadi ya Mbweni, Nd. Maulid Mwinyi Wadi ya Mombasa,
Suleiman Mussa Wadi ua Shakani na Nd. Khamis Abdillah Wadi ya Kisauni.